Kamishna wa serikali anayehusika na vyombo vya habari vya Ujerumani Wolfram Weimer, ameiambia DW kwamba Urusi inaogopa uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari kwa sababu watu wataweza kusikia na kuuona ukweli.

Mkurugenzi Mkuu wa DW Barbara Massing amesema hatua hiyo mpya ya kutengwa kwa shirika la DW itawaathiri wafanyakazi wa idhaa ya lugha ya Kirusi ya DW, ambao wengi wao wana uhusiano wa karibu na nchi yao. Lakini amesema haina tija.

Mkurugenzi Mkuu wa DW | Barbara Massing 2025
Mkurugenzi Mkuu wa DW Barbara Massing Picha: Julia Nohr Fotografie

“Urusi inaweza kutuita shirika lisilofaa nchini mwake, lakini hilo halitatukatisha tamaa. Hatua ya hivi karibuni ya kunyamazisha vyombo vya habari huru inaangazia wazi kwamba Urusi inapuuza uhuru wa vyombo vya habari na inafichua hofu yake ya kutolewa taarifa huru. Licha ya serikali ya Urusi kudhibiti na kuzuia huduma zetu, idhaa ya lugha ya Kirusi ya DW sasa inawafikia watu wengi zaidi kuliko hapo awali. Tutaendelea kuripoti kwa uhuru kuhusu vita vya uchokozi dhidi ya Ukraine na mada zingine ambazo taarifa zake zinapatikana kwa uchache nchini Urusi ili watu waweze kujenga maoni yao wenyewe.”

Idhaa ya DW ya lugha ya Kirusi imewafikia watumiaji milioni 10 kwa wiki katika mwaka huu wa 2025, wengi wao katika maudhui ya video, na kuifanya kuwa mojawapo ya idhaa10 bora za shirika la utangazaji la DW.

Naye Kamishna wa zamani wa utamaduni na Vyombo vya Habari kutoka chama cha Kijajni cha walinda mazingira. Claudia Roth, ameonyesha wasiwasi wake juu ya wafanyakazi wa DW wa idhaa ya Kirusi, familia zao na watu wanaowasiliana nao nchini Urusi. Amesema nchini Urusi, ni hatari kuripoti kwa uhuru dhidi ya mtawala wa kimabavu.

David Schliesing, wa Chama cha mrengo wa kushoto amesema, “uandishi wa habari huru si uhalifu kamwe,” lakini anaamini kwamba Urusi inaweza kuwa inajibu vikwazo vilivyowekwa dhidi ya shirika la utangazaji la serikali la Russia Today (RT) ndani ya Umoja wa Ulaya.

Taarifa ya serikali ya Urusi iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram mwishoni mwa wiki, juu ya mabadiliko hayo, ilisema ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu inaiona DW kuwa kwenye mstari wa mbele katika propaganda za uadui dhidi ya Urusi.

Urusi Moscow 2025 | Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Gavriil Grigorov/AFP

Hatua ya kufungiwa DW inazidi kuimarisha vikwazo si tu kwa shughuli za DW nchini Urusi, ambazo Moscow ilizifunga miaka iliyopita, lakini pia katika kushirikiana au kufanya kazi kwa ajili ya shirika hilo.

Watu watakaopatikana wanaunga mkono, kufanya kazi na mashirika yaliyopigwa marufuku au hata kushiriki kwenye maudhui yoyote ya DW wanaweza kukabiliwa na faini au hata kifungo jela nchini Urusi.

Shirika la DW lilianzishwa mwaka wa 1953, ni chombo huru cha habari kinachofadhiliwa na serikali ya Ujerumani, na kinachoripoti kote ulimwenguni katika lugha 32.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *