Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema vitisho vipya vya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran ni sehemu kubwa ya vita vya kisaikolojia, akisisitiza kuwa majaribio ya awali ya kuitisha Iran kwa nguvu za kijeshi au vikwazo hayakuwahi kuzaa matokeo yaliyotarajiwa.

Katika mahojiano maalum na Al Jazeera yaliyotolewa kwa ukamilifu Jumanne, mwanadiplomasia huyo mkuu alisema taarifa za uwezekano wa shambulio jipya la Israel zinalenga “kuibua hofu na msisimko wa taharuki ndani ya nchi.”

Alibainisha kuwa vitisho hivyo si jambo jipya, akirejea miongo ya onyo kutoka Marekani na utawala wa Israel kwamba “chaguzi zote ziko mezani,” ikiwemo mashambulizi ya kijeshi.

Kwa mujibu wa Araghchi, hata hivyo, wananchi wa Iran wamezoea mbinu hiyo. “Kwa miaka mingi, pengine miongo, Wamarekani na Waisraeli wamekuwa wakitoa vitisho kama hivyo,” alisema, akisisitiza kuwa lengo lake ni “kuchochea wasiwasi na hofu katika jamii.”

Amekumbusha kuwa vita vya kichokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran mwezi Juni vilionyesha wazi jinsi hatua ya kijeshi ilivyoshindwa kufikia malengo yake yaliyotangazwa.

Amesisitiza kuwa ukatili wa siku 12 ulikuwa “jaribio lililofeli.”

Akitolea mfano, amekumbusha kuwa katika mashambulizi hayo tawala za Tel Aviv na Washington zilitumia ndege zao kubwa zaidi, ndege za kivita za kisasa zaidi, na mabomu yao yenye nguvu zaidi dhidi ya vituo vya nyuklia vya chini ya ardhi vya Iran bila kufanikiwa.

Akinukuu kauli ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, Araghchi amesema teknolojia ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu imebuniwa ndani ya nchi, hivyo uharibifu wowote unaweza kurejeshwa na wanasyansi wa Wairani.

Waziri huyo aliongeza kuwa Iran haipuuzi uwezekano wa vita vipya, akisisitiza kuwa nchi iko tayari kujilinda katika hali yoyote. “Uwezekano wa vita umekuwepo daima na bila shaka upo hata sasa,” alisema, akiongeza kuwa Jeshi la Iran na wananchi “wako tayari kikamilifu” kulinda nchi.

Araghchi amesema taasisi za usalama za Iran huendelea kuchambua matukio yanayoweza kutokea na kuwapa viongozi wakuu taarifa za mara kwa mara ili kuhakikisha utayari wa kila hali.

Akiashiria vita vya mauaji ya kimbari vinavyofanywa na Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza kwa msaada wa Magharibi, amesema Iran inakabiliana na mahasimu “wasio na mipaka katika uhalifu wao.”

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *