
Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, ameitaja Iran kuwa mfano bora duniani katika kutetea sheria za kimataifa, akishukuru Jamhuri ya Kiislamu kwa msimamo wake thabiti wa kuiunga mkono Caracas wakati ambapo vitisho kutoka Marekani vinaongezeka.
Akizungumza katika kipindi chake cha televisheni cha kila wiki, “Con Maduro”, kiongozi huyo amepongeza msimamo wa Iran ambao ameuona kuwa wa uthabiti na wa kimsingi katika medani ya kimataifa.
Alitoa maelezo kuhusu mazungumzo yake ya simu na Rais Masoud Pezeshkian, akisema aliarifiwa kuhusu uungaji mkono kamili wa Iran kwa uhuru na uthabiti wa Venezuela.
Maduro amesema Rais Pezeshkian alimfahamisha kuhusu “uungaji mkono mpana na usio na shaka” kutoka kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, serikali na wananchi wa Iran kwa taifa la Venezuela.
Maduro amesema: “Naposema uungaji mkono mpana, namaanisha wa jumla na usio na masharti.” Aidha amebainisha kuwa msaada huo utatoa msukukumbo katika mapambano ya Venezuela kwa ajili ya amani, uhuru, heshima na uthabiti, “si kwa leo au kesho tu, bali milele.”
Rais Maduro amesisitiza kuhusu nafasi muhimu ya Iran katika masuala ya kimataifana kusema kuwa: “Jamhuri ya Kiislamu ni “mfano angavu katika jitihada za kuanzisha utawala wa sheria kimataifa,” na akamshukuru rais wa Iran kwa msimamo thabiti wa Tehran.
Serikali ya Marekani imeongeza shinikizo dhidi ya Venezuela kupitia kwa kuongeza majeshi yake katika eneo la Karibiani, ikidai bila ushahidi kuwa inafanya operesheni dhidi ya usafirishaji wa dawa za kulevya.
Tangu Septemba, Marekani imefanya angalau mashambulizi 21 dhidi ya meli zinazodaiwa kubeba dawa za kulevya katika Bahari ya Karibiani na Pasifiki, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 83.
Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara uungaji mkono wake kwa uhuru, usalama na uthabiti wa Venezuela mbele ya shinikizo na mashambulizi ya Marekani.
Iran na Venezuela, ambazo ni washirika wa muda mrefu wa kimkakati, zinaendelea kusisitiza umuhimu wa kukabiliana na uonevu wa upande mmoja na vikwazo visivyo vya haki vya Magharibi, huku zikiendeleza ushirikiano wa karibu katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia.