Takribani watu 30, wengi wao wakiwa walimu, wamefariki huku kadhaa wakiripotiwa kupotea baada ya boti kuzama katika mto ulioko jimbo la Kwilu, magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ajali hiyo ilitokea mwishoni mwa wiki katika Mto Kwango, lakini mamlaka ziliithibitisha tukio hilo kwa vyombo vya habari siku ya Jumatano.

Kwa mujibu wa mbunge wa eneo hilo, Gary Sakata, boti hiyo ilikuwa imebeba takribani abiria 100 kutoka vijiji vya Kingukukapayi, Kusu na Fambondo, katika eneo la Bagata.

Sakata aliambia redio Top Congo kwamba: “Waliokufa ni pamoja na walimu 20 waliokuwa wakielekea mjini Bandundu kwenda kuchukua mishahara yao ya mwezi, huku wasafiri wengine wakiwa njiani kwenda kufanya manunuzi kuelekea sherehe za mwisho wa mwaka.”

Mbunge huyo alikosoa mfumo “usiofanya kazi ipasavyo” wa ulipaji mishahara kwa watumishi wa umma vijijini, akisema: “Hatuwezi kupoteza walimu 20, sawa na shule mbili, kwa sababu walilazimika kusafiri zaidi ya kilomita 100 kwenda kuchukua mishahara yao.” Abiria 30 waliokolewa.

Inadaiwa kuwa boti hiyo, ambayo pia ilikuwa imebeba mifuko 700 ya saruji na mihogo, iligonga kitu kilichokuwa kimezama na hakisogei, na kusababisha izame.

Usafiri wa maji ni hutegemewa sana nchini DRC  kutokana na barabara nyingi kutopitika, na ajali za aina hii hutokea mara kwa mara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *