Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amelaani jinai zinazoendelea kufanywa na Israel huko Ghaza na mashambulizi yake dhidi ya Lebanon, na amezitaka nchi za ukanda huu na jamii ya kimataifa ichukue hatua kali za kukabiliana na tishio la mara kwa mara la utawala wa Kizayuni dhidi ya amani na utulivu wa eneo hili na dunia nzima kwa ujumla.
Akigusia mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza kupitia mashambulizi ya kikatili na kuzuia kuingia misaada ya kibinadamu kwenye ukanda huo, Ismail Baghaei, amekumbusha kuwa, jukumu la jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka na madhubuti za kukomesha uhalifu huo na kuwashtaki wahalifu wa kivita na wahusika wa mauaji ya kimbari.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amezungumzia pia azimio la hivi karibuni la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu ushauri wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ambayo ilisisitizia wajibu wa mataifa yote, kwa mujibu wa Kifungu cha 1 cha Mikataba ya Geneva ya 1949, kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na kulaani vikali ukiukwaji wa mara kwa mara na mkubwa wa sheria za kibinadamu na utendakazi wa jinai za kivita, jinai dhidi ya binadamu na mauaji ya umati yanayofanywa na utawala wa Kizayuni, na kusisitizia haja ya kukomeshwa kiburi cha utawala wa Kizayuni.
Baghaei amesema kuwa, Marekani na makundi ya Kizayuni wanashirikiana kufanya mauaji ya umati ya Wapalestina na jinai nyingine zinazofanywa na utawala huo pandikizi katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu pamoja na katika nchi za Lebanon na Syria, na amesema: Licha ya kutangazwa madai ya kusitisha mapigano huko Ghaza na Lebanon, lakini utawala wa Kizayuni, kwa msaada kamili wa Marekani na kutojali makubaliano ya kusitisha vita.

Hapana shaka kuwa, kuwafungulia mashitaka viongozi wa utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) au kuanzisha mahakama maalumu kunaweza kuzuia kukaririwa jinai na kutuma ujumbe wa wazi kwa wanaokiuka haki za binadamu duniani kote.
Harakati maarufu na mashirika ya kutetea haki za binadamu kote duniani yanatoa mwito wa uwajibikaji kutoka kwa utawala wa Kizayuni, jambo ambalo linaweza kufungua njia ya kuchukuliwa hatua za kisheria za kimataifa.
Hata hivyo, kushtakiwa kwa viongozi wa utawala wa Kizayuni katika mahakama za kimataifa kunakabiliwa na vikwazo vikubwa, kutokana na msaada wa kisiasa na kidiplomasia kutoka Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi, udhaifu wa kimuundo wa mfumo wa sheria za kimataifa na ukosefu wa nyenzo madhubuti za utekelezaji athirifu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mambo ambayo kimsingi yanazuia utekelezaji wa hukumu na ufuatiliaji wa kisheria.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) haina utaratibu huru wa utekelezaji na inategemea ushirikiano wa serikali kutekeleza hukumu zake. Fauka ya hayo mataiifa mengi ikiwemo Marekani na serikali za Magharibi, ambazo hazitoi ushirikiano unaohitajika wa kuwarejesha washtakiwa au kutekeleza hukumu.
Marekani ikiwa muungaji mkono sugu wa utawala wa Kizayuni katika Baraza la Usalama, inatumia kura yake ya veto kuzuia kupitishwa kwa azimio lenye nguvu kisheria. Katika baadhi ya matukio, serikali ya Marekani hata imeweka vikwazo dhidi ya majaji na waendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ili kuvuruga taratibu za ushughulikiaji wa mafaili dhidi ya Israel na washirika wake. Serikali nyingi za Magharibi, zikihofia madhara ya kisiasa na kiuchumi, hujiepusha kuunga mkono hadharani mashtaka dhidi ya viongozi wa utawala wa Kizayuni.
Uungaji mkono wa Marekani na nchi za Magharibi, udhaifu wa kimuundo wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, mchakato mrefu wa kesi, na kutokuwa mwanachama kwa utawala wa Kizayuni katika mahakama hizi vyote vinazuia utekelezaji wa haki. Hata hivyo, kuwasilisha malalamiko na kutoa hukumu, hata kama hazitekelezwi, kuna umuhimu wa kinembo na kisiasa na kunaweza kudhoofisha uhalali wa utawala wa Kizayuni duniani kote.

Licha ya ukwamishaji mambo wote uliofanywa na Marekani na nchi za Magharibi kwa kuunga mkono utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa na katika mahakama za kimataifa, lakini ulimwengu wa Kiislamu unaweza, kwa kutumia uwezo wa kisheria wa kimataifa, umoja wa kisiasa na kidiplomasia, kwa kuunda kamati za pamoja na shinikizo la umma, kuandaa mazingira ya kesi dhidi ya viongozi wa utawala wa Kizayuni katika mahakama za kimataifa.
Kuna mifumo ya kisheria ya kuushtaki utawala wa Kizayuni katika majukwaa ya kimataifa, lakini utekelezaji wake unahitaji umoja wa nchi za Kiislamu, mashinikizo ya umma, uandikishaji makini wa uhalifu na matumizi ya uwezo wa kisheria uliopo.
Kutokana na ukatili unaoendelea wa Wazayuni huko Gaza, wanaharakati wengi wa asasi za kiraia na taasisi za kitaaluma duniani kote, ikiwemo Marekani na Ulaya, wameongeza juhudi zao ili kuhakikisha kwamba, viongozi wa utawala wa Kizayuni wanashtakiwa katika mahakama za kimataifa.