Miezi miwili inakaribia kumalizika tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumanne, Oktoba 28 na Jumatano, Oktoba 29 kwa Zanzibar.

Uchaguzi huo uliacha nyuma yake wingu zito la malalamiko na madai kuwa matokeo yaliyotangazwa hayawakilishi uamuzi wa kweli wa wapigakura.

Kwa sasa, hali inaonekana kuwa tulivu, lakini ukimya huo hauondoi hisia kwamba mengi yanaendelea kufanyika kwa siri na hata kwa uwazi. Dalili zote zinaashiria kuwa utulivu unaoonekana huenda ni wa juu juu, huku chini kukiwa na mvutano unaofukuta polepole.

Wapo wanaoamini kuwa kinachopaswa kufanywa ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa uchaguzi ulimalizika bila vurugu kubwa, kisha wananchi waelekeze nguvu zao mbele katika kujenga nchi.

Kwa mtazamo huo, yaliyopita yapaswa kusahaulika ili jamii isonge mbele. Hata hivyo, kwa upande mwingine, kuna kundi kubwa la wananchi na wadau wa siasa wanaoamini kuwa suala la uchaguzi halijafungwa na kwamba, madai ya mizengwe na wizi wa wazi wa kura hayawezi kufunikwa kwa ukimya.

Hali hii inaweza kufananishwa na bakuli la uji ambalo juu linaonekana kuwa baridi, lakini ukivuta fundo unakutana na joto kali linaloweza hata kubabua ulimi.

Kutokuwapo kwa vurugu hakupaswi kuchukuliwa kama kielelezo cha kuwapo kwa maridhiano, kuaminiana au kuelewana. Kufikiri hivyo ni kujidanganya, kwa sababu hasira, masikitiko na hisia za kudhulumiwa bado zipo miongoni mwa wananchi.

Hasira hizo zimejitokeza kwa njia mbalimbali, ikiwamo hatua ya chama cha ACT – Wazalendo kufungua kesi zaidi ya 20 mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi.

Hatima ya kesi hizo itajulikana siku zijazo, lakini tayari kuna mashaka miongoni mwa wananchi kama zitasikilizwa na kuamuliwa kwa wakati unaostahiki.

Mashaka hayo yanatokana na historia ya kesi za uchaguzi nchini, ambazo baadhi yake zimechukua miaka mingi bila uamuzi, au ziliachwa bila kusikilizwa kabisa.

Hata hivyo, si busara kuwahukumu mahakimu waliopo sasa kwa kuwaweka katika kundi moja na waliopita. Ni vyema kusubiri na kuona namna haki itakavyotendeka katika mazingira ya sasa.

Pamoja na hilo, si hekima kupuuza hasira za wananchi kuhusu namna uchaguzi ulivyoendeshwa, hasa kutokana na madai mazito ya watoto wadogo kupiga kura, baadhi ya watu kupiga kura zaidi ya mara moja, pamoja na ukosefu wa uwazi katika zoezi la kuhesabu kura na kutangaza matokeo.

Hasira hizi zimefikia hatua ambayo wengi hawakuitarajia, kwa kuwa katika historia ya siasa za Zanzibar haijawahi kushuhudiwa kwa kiwango hiki. Katika baadhi ya maeneo, wananchi wamechukua hatua ya kufanya kisomo cha dua maalumu kinachoheshimiwa sana katika Uislamu, kiitwacho Hizb al-Badri, ambacho hufanywa na mtu au kundi linaloamini kuwa limedhulumiwa na kumwachia Mwenyezi Mungu suala lao.

Kwa waumini wa Kiislamu, hatua hii si jambo dogo, kwa kuwa masharti yake ni kuhakikisha kuwa anayekisoma kweli amedhulumiwa na anatafuta haki kupitia kwa Mungu.

Wakati kesi zikiendelea mahakamani, wapo wanaopendekeza kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza namna uchaguzi ulivyoendeshwa na jinsi matokeo yalivyopatikana.

Wengine wanapinga wazo hilo wakidai kuwa suala likiwa mahakamani, kuunda tume kama hiyo ni kinyume na misingi ya utawala bora. Hata hivyo, hoja hiyo inapigwa vita kwa mifano ya Tanzania Bara, ambako licha ya kuwepo kwa kesi mahakamani, bado tume maalumu ziliundwa kuchunguza vurugu za uchaguzi, jambo linaloonyesha kuwa hatua hizo mbili zinaweza kwenda sambamba.

Sambamba na hayo, kunasikika wito wa maridhiano kati ya vyama viwili vinavyokinzana zaidi, CCM na ACT – Wazalendo. Kwa misingi ya kijamii na kisiasa, maridhiano ni jambo jema, kwani mfarakano wowote unahitaji suluhu inayojengwa juu ya maelewano na nia ya kusonga mbele kwa pamoja.

Hata hivyo, maridhiano ya kweli hupatikana pale pande zote zinapokiri kuwepo kwa tatizo. Swali linalojitokeza ni iwapo CCM na ACT wote wanakubali kwamba kuna tatizo linalohitaji suluhu.

Mashaka yanaongezeka kutokana na historia ya makubaliano ya mwafaka yaliyofikiwa mara kadhaa huko nyuma, lakini baadaye kuvunjika au kutotekelezwa ipasavyo.

ACT – Wazalendo imekuwa ikidai kuwa makubaliano mengi hayakutekelezwa na kwamba, hali ya kutojali washirika wake ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa imekuwa mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya mwafaka.

Kwa hali hiyo, Zanzibar bado inakabiliwa na kitendawili kikubwa cha kupata Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya kweli, inayojengwa juu ya uaminifu na kuheshimiana. Ingawa methali ya Kiswahili yasema penye nia pana njia, bado njia hiyo haijaonekana wazi.

Kinachobaki ni kumwomba Mwenyezi Mungu ajaalie joto la kisiasa lililopo Zanzibar lipungue, haki itendeke au angalau mwelekeo wa dhuluma inayodaiwa upunguze makali ya maumivu kwa umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *