Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba awajia juu wanaolaumu wasanii kushiriki kwenye kampeni za CCM.

Akizungumza leo Jumatano, Desemba 17, 2025 alipokuwa anakagua uharibifu katika soko la Machinga na kusalimia wananchi, Tunduma mkoani Songwe amesema wasanii kuimba kwenye kampeni ni sehemu ya ajira yake inayompatia kipato.

“Tuna mambo mengi leo nilipita kusalimia tu. Mtu anakaa huko sijui kwenye nchi yake ameshapata uraia kisa anaongea kiswahili, mwingine amehifadhiwa huko. Eti anawaambieni wasanii wakataeni walienda kwenye kampeni za CCM. Ajira ya msanii si sanaa unataka mtu aache ajira yake.

“Nani kawaambia wachezaji wanaocheza Manchester ni mashabiki wa Manchester. Nani kawaambia watu wanaocheza Simba ni mashabiki wa Simba uchezaji ni ajira yao. Msanii akienda kuimba yeye pale yupo kazini, yupo kwenye ajira yake. Tunahangaika vijana wapate wewe unasema wakatae fursa ya kupata fedha,” amesema.

Amesema Watanzania wasikubali kupandikizwa chuki zisizo na msingi.

“Nani kawaambieni hao ni wanachama, nani kawaambia wanaenda kuimba kwa kadi, nani kawaambieni nyimbo za kwaya zinatengenezwa kwenye studio za walokole. Yule aliyetengeneza nyimbo hizo nani kawaambia kaokoka? Hawa wana akili au kamasi, mnakataa watu wasifanye kazi?

“Na kuna watu tunaanza kushabikia hilo, tunapelekwa wapi chuki za kijinga hizo kama mtu anaandaa mkutano au harusi yake anamlipa msanii wewe kinakuuma nini yeye ni ajira yake. Ana somesha watoto ana kodi ya nyumba anaipatia kwa kipaji hicho mbona mnapangiwa tofali moja moja la chuki, na nyie mnafurahia mambo gani hayo ya hovyo?  Yaani ndio nchi ambayo Mwalimu Nyerere alituachia hii, alituachuia nchi ambayo hatuulizani kabila wala dini,” amesema. 

Utakumbuka kauli hii ya Waziri Mkuu imekuja kukiwa na mgogoro kati ya wasanii na baadhi ya mashabiki wanaowatuhumu wasanii kutoshiriki kwenye masuala ya kijamii. Hivyo basi wameamua kutounga mkono kazi za wasanii hao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *