Meneja wa Chelsea, Enzo Maresca, ameelezea furaha yake baada ya kuimbiwa na mashabiki wa klabu hiyo kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Cardiff City ulioivusha Chelsea kwenda hatua ya nusu fainali ya Kombe la Carabao.

Maresca alipata heshima kubwa kutoka kwa mashabiki wa Chelsea waliokuwa ugenini baada ya filimbi ya mwisho, hali iliyokuja siku chache baada ya kauli yake kuwa saa 48 kabla ya ushindi wa Everton yalikuwa magumu zaidi tangu ajiunge na klabu hiyo.

Akizungumza baada ya mchezo, Maresca amesema furaha yake kubwa ni kufuzu nusu fainali, akisisitiza kuwa hilo ndilo jambo linalowaridhisha mashabiki.

“Nina furaha tu. Tupo nusu fainali na naamini ni kitu ambacho mashabiki wanastahili. Ilikuwa ni wakati mzuri sana, nawathamini na nashukuru,” amesema Maresca.

Alikiri kuwa kuna nyakati mashabiki huonyesha kutoridhika pale matokeo yanapokosekana, lakini akasisitiza kuwa kwa ujumla wamekuwa wakimuunga mkono.

“Hizi ni mechi ambazo zinanifanya niwapende zaidi wachezaji wangu, kwa sababu ni rahisi sana kuteleza lakini ni michezo ya hatari. Kila msimu kuna timu zinazotolewa na klabu za ligi daraja la kwanza au la pili. Lazima tuwe makini,” ameongeza.

Chelsea ilibadili sura kipindi cha pili baada ya kuwaingiza, Alejandro Garnacho na Pedro Neto, ambao walibadili mwelekeo wa mchezo. Garnacho alifunga mabao mawili huku Neto akiongeza lingine.

Hata hivyo, Cardiff ilitoa upinzani mkali baada ya David Turnbull kusawazisha kwa bao la kichwa dakika 15 kabla ya mpira kumalizika, bao lililorejesha matumaini kwa Cardiff lakini matumaini hayo yalizimwa baada ya Chelsea kuibuka na ushindi katika dakika za mwisho.

Akizungumzia kauli zake za awali na uhusiano wake na uongozi wa klabu, Maresca amesema hajazungumza na viongozi wa Chelsea tangu mwishoni mwa wiki, akisisitiza kuwa akili yake ipo kwenye mechi zijazo.

“Baada ya Everton nilianza maandalizi ya Cardiff. Sasa tunaanza maandalizi ya Newcastle. Hakuna muda wa mambo mengine,” amesema.

Maresca pia amethibitisha kuwa winga wa Brazil, Estêvão, atakosekana kwenye mchezo dhidi ya Newcastle kutokana na kusumbuliwa na tatizo la misuli.

Kwa upande wa Cardiff, kocha Brian Barry-Murphy amesema bao la kusawazisha liliwapa matumaini makubwa, lakini tofauti ya ubora ndiyo imefanya wapoteze mchezo.

“Ni matumaini yanayokuua unapofunga bao. Tulikuwa na nafasi ya kufanya jambo kubwa, lakini haikuwezekana. Mashabiki walikuwa nasi hadi dakika ya mwisho,” amesema Barry-Murphy.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *