Katika kuendelea kuimarisha sekta ya ujenzi visiwani Zanzibar, Benki ya NMB imezindua maboresho yenye suluhisho maalumu kwa ajili ya makandarasi zikilenga kuziwezesha kampuni za ndani kufanya miradi mikubwa.
Hatua hiyo inalenga kuwawezesha kuwa sehemu ya kuchangia uchumi wa Taifa na maendeleo ya haraka kupitia miradi mikubwa ya ujenzi.
Hafla hiyo ya uzinduzi imefanyika Jumanne Desemba 16, 2025 katika Hoteli Verde visiwani huko ikiwaleta pamoja viongozi muhimu wa Serikali, kisekta na kundi kubwa la makandarasi kutoka kote visiwani.
Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohamed, ambaye alisisitiza nia kubwa ya Serikali katika kukuza sekta hii muhimu ya ujenzi, huku ujumbe wa NMB uliongozwa na Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa benki hiyo, Filbert Mponzi, ambaye ndiye aliyelezea mabadiliko hayo makubwa.
Dk Khalid ameshukuru mpango huo wa NMB uliokuja wakati muafaka na ambao ulikuwa unahitajika huku akisisitiza umuhimu wa maboresho haya kwa mustakabali wa maendeleo ya Zanzibar.
“Hii si tu ishara ya nia njema; ni uwekezaji wa kimkakati katika msingi wa maendeleo yetu ya kitaifa, tuna kila sababu ya kuishukuru na kuipongeza NMB,” amesema Dk Khalid.
Pia ametumia fursa hiyo kuwasihi makandarasi waliokuwepo kuhakikisha wanatumia fursa hizo kutoka kwa NMB kwa ajili ya kuendelea kuwa bora na kuweza kujipatia tenda kubwa, ambazo mara nyingi zimekuwa zikienda kwa makandarasi wa nje ya nchi kwa sababu ya ukubwa wa mtaji walio nao.
Hivyo uwepo wa NMB unakwenda kuwa suluhisho kwa makandarasi kujipatia tenda hizo.
Waziri huyo amesisitiza zaidi juu ya azma ya Serikali kwa makandarasi wa ndani kushiriki kikamilifu katika miradi ya kimkakati ikiwa pia ni moja ya maono ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi kuona makandarasi wazawa ndio wanaoshiriki katika miradi mikubwa Zanzibar.
“Ndugu zangu makandarasi, nawaomba mfike katika matawi ya NMB huko Unguja na Pemba, mkumbatie fursa hizi, na kuzitumia kwa manufaa makubwa ya biashara zenu na ukuaji wenu binafsi. Dhamana hizi zitawawezesha kushindana kwa zabuni kubwa zaidi, ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikihodhiwa na taasisi za kigeni,” amesema.
Kwa upande mwingine, Mponzi amesisitiza ahadi ya benki hiyo katika kusaidia ukuaji wa makandarasi wa ndani.
Amesema maboresho hayo ni matokeo ya utafiti wa kina juu ya uwezo wa kiuchumi wa makandarasi na changamoto za wazi wanazokabiliana nazo katika kupata zabuni, mara nyingi kutokana na mapungufu ya uwezo wa kifedha.
“Tulitambua kuwa uwezo wa kupata fedha na dhamana mara nyingi ndio kikwazo kikuu kinachowazuia makandarasi wetu ambao tunaamini wana uwezo mkubwa wa kushindana na kushinda miradi mikubwa. Kwa ushirikiano mkubwa na benki yetu, wazawa watapata miradi hii mikubwa,” amesema Mponzi.
Msingi wa maboresho haya kutoka Benki ya NMB unatokana na ongezeko kubwa la dhamana za kifedha. Benki hiyo imeongeza dhamana ya juu zaidi ya Bid Bond (Bid Bond Guarantee) kutoka Sh2.5 bilioni hadi Sh25 bilioni, na muhimu zaidi, kiasi hiki kilichoongezeka kinapatikana bila hata dhamana. Hatua hii inatarajiwa kufungua milango kwa makandarasi kushindana kwa miradi mingi zaidi ya umma na binafsi ambayo hapo awali ilikuwa nje ya uwezo wao.
Zaidi ya hayo, NMB imeongeza kwa kiasi kikubwa kiwango cha juu cha Dhamana za Miradi, ikiwemo Dhamana za Utendaji (Performance Guarantees) na Dhamana za Malipo ya Awali (Advance Payment Guarantees). Makandarasi sasa wanaweza kupata hadi Sh3 bilioni kwa kila mradi bila dhamana, hasa kwa taasisi zote za Serikali ya Zanzibar kama vile Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), na wizara mbalimbali.
Hii inaashiria ongezeko kubwa kutoka kikomo cha awali cha Sh1.5 bilioni ikitoa msaada muhimu wa kifedha kwa utekelezaji wa miradi na uhamasishaji wa awali.
“Kwa miradi ya kimkakati ya miundombinu kama barabara, majengo, na wasambazaji maalumu kwa Wizara ya Uchumi wa Bluu, benki iko tayari kutoa viwango vya juu zaidi, vinavyozidi Sh3 bilioni bila dhamana,” Mponzi aliongeza.
Boresho jingine muhimu lililotangazwa kwa makandarasi wakati wa hafla hiyo ni ugatuzi wa michakato ya idhini.
Ili kuharakisha utoaji wa huduma, mameneja wa matawi ya NMB kote nchini sasa wamewezeshwa kuidhinisha maombi yote ya Bid Bond, Performance, na Advance Payment Guarantee hadi Sh500 milioni bila kuhitaji dhamana. Ugatuzi huu wa kimkakati unalenga kupunguza kwa kiasi kikubwa muda wa utekelezaji (TAT), ambapo maombi hadi kiwango hiki sasa yatashughulikiwa ndani ya saa 24-36, ikiwa nyaraka zote muhimu zimekamilika. Kwa maombi makubwa zaidi yanayozidi Sh500 milioni, maamuzi yatatolewa katika makao makuu ya benki ndani ya siku 10 za kazi.
Akizungumza, Mjumbe wa Bodi ya Usajili Makandarasi Zanzibar (ZCRB), Mhandisi Kassim Ali Omary, ameipongeza NMB kwa juhudi zake kama hatua muhimu kuelekea uwezeshaji wa kiuchumi wa ndani.
Maboresho ya Benki ya NMB yanatarajiwa kubadilisha mazingira kwa makandarasi Zanzibar, ikiwawezesha kuwa na ari ya kufanya kazi yenye tija zaidi katika uimara wa uchumi wa Zanzibar.