Kauli ya kwamba Urusi itafanikisha malengo yake ya kivita nchini Ukraine imetolewa siku ya Jumatano na Rais Vladimir Putin mwenyewe alipokuwa akifanya mazungumzo na maafisa wa wizara ya ulinzi mjini Moscow na kusema “kwa hakika” watayanyakua maeneo waliyoyadhamiria. Putin amesema anatoa kipaumbele kwa michakato ya kidiplomasia ili kuutatua mgogoro huo, lakini akasisitiza kuwa hilo linaweza pia kufanikiwa kwa “kutumia nguvu za kijeshi”.

Hata hivyo, kulingana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, bado kuna mivutano kuhusu ni maeneo gani Ukraine italazimika kuyaachia kwa Urusi. Pendekezo la awali la Marekani lililoandaliwa bila kuwashirikisha  washirika wa Ulaya  linaitaka Ukraine kujiondoa katika eneo lake la mashariki mwa Donetsk na pia Marekani kuyatambua rasmi maeneo ya Donetsk, Rasi ya Crimea na Lugansk kama maeneo ya Shirikisho la Urusi.

Mara kadhaa mataifa ya Ulaya yameonekana kulipinga hilo, lakini hivi karibuni yamesikika yakisema kuwa yataheshimu uamuzi utakaochukuliwa na Ukraine. Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Italia Georgia Meloni amesema kupitia mpango huu wa amani  unaosimamiwa na Marekani, Urusi inawasilisha matakwa “yasiyo na uwiano.”

“Hili linadhihirishwa na mashambulizi yasiyoisha kwenye miji na miundombinu ya Ukraine, na pia dhidi ya watu wasio na ulinzi, na kuthibitishwa na madai yasiyo na msingi ambayo Moscow inayawasilisha kwa wadau wenzake, hasa kuhusu eneo la Donbass ambalo bado halijanyakuliwa na Urusi.”

Azma ya pande zote ya kuumaliza mzozo huu

Berlin | Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akiuhutubia mkutano wa Berlin
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akihutubia mkutano wa Berlin uliokuwa ukijadili mzozo kati ya Kiev na MoscowPicha: Emmanuele Contini/NurPhoto/picture alliance

Pande zinazopigana zinaonekana kujaribu kulegeza kamba ili kuwezesha mpango huu kufanikiwa. Ukraine ilitangaza kuwa tayari kuachana na azma yake ya kujiunga na  Jumuiya ya Kujihami ya NATO  na kuonekana kuwa tayari kuyaachia baadhi ya maeneo, huku Urusi nayo ikiashiria nia ya kujadili uwezekano wa kupelekwa kwa wanajeshi wa nchi za Magharibi nchini Ukraine baada ya usitishwaji mapigano, licha ya upinzani wake wa muda mrefu dhidi ya hatua kama hiyo.

Licha ya juhudi hizo za kidiplomasia, bado mapambano yanaendelea. Mkuu wa Jeshi la Ukraine Oleksandr Syrskii, amesema siku ya Jumatano kuwa vikosi vya Ukraine vimefanikiwa kuchukua udhibiti wa karibu asilimia 90 ya mji wa kaskazini mashariki wa Kupiansk. Lakini Waziri wa Ulinzi wa Urusi Andrei Belousov, amesema vikosi vya Ukraine vilikuwa vikijaribu kuchukua udhibiti wa mji huo, ingawa juhudi zao hadi sasa hazijafanikiwa.

(Vyanzo: DPA, AFP, RTR)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *