Wakenya hao ambao waliingia nchini humo kama watalii walikutwa wakiwaandikisha WaAfrika Kusini Wazungu, ambao wanaomba hifadhi ya ukimbizi kupitia mpango wa serikali ya Marekani, kwa madai ya kunyanyaswa na utawala wa Waafrika Kusini Weusi. 

Kulingana na mamlaka za Afrika Kusini, Wakenya hao ambao hawakuwa na nyaraka zinazowaruhusu kufanya kazi nchini humo, waliajiriwa na shirika moja lisilo la serikali nchini Kenya ambalo lilipewa mkataba wa kuwasajili raia Wazungu wa Afrika Kusini wanaotaka kuomba uhifadhi ya ukimbizi nchini Marekani.

Waafrikaner kutoka Afrika Kusini wakiwasili Marekani kwa ajili ya kupewa makazi
Utawala wa Rais Trump ulitangaza mpango wa kutoa hifadhi za ukimbizi kwa raia Wazungu wa Afrika KusiniPicha: Saul Loeb/AFP

Kukamatwa kwa Wakenya hao Jumanne kulifuatia upelelezi na uvamizi katika kituo kimoja cha kushughulikia maombi ya wakimbizi na walikutwa wakiandaa nyaraka za visa ili waweze kwenda Marekani. Maafisa wa Afrika Kusini wamesema kuwa watu hao hawakukamatwa kwenye eneo la kidiplomasia kama walivyodai maafisa wa Marekani.

Mwezi Oktoba mwaka huu utawala wa Rais Trump ulitangaza mpango wa kutoa hifadhi za ukimbizi kwa raia Wazungu wa Afrika Kusini maarufu kama Afrikaner wapatao 7,500 katika mwaka huu wa kifedha. Idadi hii ni chini ya ile iliyokuwa imepangiwa ya watu 100,000 chini ya utawala wa Rais Joe Biden. Baada ya hapo kundi la takribani watu 50 walifanikiwa kuhamia Marekani chini ya mpango huo. Na tangu wakati huo, vikundi vidogo vidogo vimekuwa vikiondoka Afrika Kusini chini ya mpango huo.

Uhusiano kati ya serikali za Marekani na Afrika Kusini umeendelea kuzorota tangu Rais Trump aliporudi madarakani akikosoa uongozi wa Pretoria kwa sera ambazo zinakandamiza raia hao Wazungu. Mwezi Machi mwaka huu, Marekani ilimtimua balozi wa Afrika Kusini na pia kuongeza kodi ya asilimia 30 kwa bidhaa zinazotoka kwenye nchi hiyo.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akiteta na mwenyeji wake Rais Donald Trump wa Marekani katika Ikulu ya White House
Uhusiano kati ya serikali za Marekani na Afrika Kusini umeendelea kuzorota tangu Rais Trump aliporudi madarakaniPicha: Jim Watson/AFP/Getty Images

Kufuatia kukamatwa kwa Wakenya hao, Ziraza ya Mambo ya Nje ya Marekani imeshutumu vikali kisa hicho. Naibu Msemaji wa wizara hiyo, Tommy Pigott katika taarifa kwa vyombo vya habari ameilezea hatua ya Afrika Kusini kuwa inaingilia shughuli zake na akasema jambo hilo halikubaliki hata kidogo.

Kwa upande wake serikali ya Afrika Kusini imewasiliana pia na ile ya Kenya kutoa ufafanuzi kuhusu hatua yake ya kuwafukuza raia wake saba ambao waliokuwa na visa za utalii pekee, jambo linalokiuka wazi masharti yao ya kuingia nchini humo na kufanya kazi.

Aidha, Wakenya hao walikamatwa na kupewa amri za kufukuzwa nchini humo, na watapigwa marufuku ya kuingia Afrika Kusini tena kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Rais wa Marekani Donald Trump
Marekani inaukosoa uongozi wa Afrika Kusini kwa sera ambazo inasema zinakandamiza raia Wazungu walio wachache. Picha: Jim LoScalzo/Pool via CNP/AdMedia/IMAGO

Mara kwa mara Rais Trump ameishutumu Afrika Kusini kwa kuwanyanyasa jamii ya walio wachache ya Afrikaner tangu utawala ulipoangukia mikononi mwa Waafrika Kusini Weusi walioishi kwa muda mrefu chini ya utawala wa ubaguzi wa rangi.

Afrika Kusini imekuwa ikikanusha vikali madai hayo ikisema kuwa Waafrika Kusini Weusi ndiyo bado wanabaguliwa pakubwa na Wazungu, kwani sera za kiuchumi bado zinaipendelea jamii hiyo.

Mvutano kati ya nchi hizo mbili ulisababisha Marekani kuususia mkutanowa kilele wa kundi la nchi tajiri na zinazoinukia kiuchumi za G20 ambao Afrika Kusini ilikuwa mwenyeji mwezi uliopita wa Novemba. Baada ya Marekani kuchukua urais wa mwaka mmoja wa G20, ilisema kuwa Afrika Kusini haitaalikwa kwenye mikutano itakayofanyika nchini Marekani mwaka ujao wa 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *