Dar es Salaam. Ukweli ni kwamba kipindi cha mwisho wa mwaka viwanja mbalimbali vya starehe husongwa na wingi watu, wakitumia pesa zao walizotafuta tangu Januari. Lakini licha ya starehe zote hizo watoto hujikuta wakisahaulika na badala yake hushinda tu nyumbani.

Kama ilivyo kwa wazazi kutumia likizo kama sehemu ya mapumziko na starehe ni vyema pia watoto wakastareheka na kujifunza. Kwa kushiriki kwenye Kids’ Holiday Festival ambayo itafanyika Dar es Salaam Desemba, 20, 2025 na Moshi Desemba 27, 2025.

Likizo inapaswa kuwa ya kujifunza na kufurahi, ndiyo maana Benki ya CRDB imeingia mkataba wa kushirikiana na Kids’ Holiday Festival kuandaa matamasha hayo ya watoto yatakayowakutanisha watoto na wazazi au walezi pamoja na kuwapa elimu ya fedha. 

Akizungumza kwenye hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano hayo, Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili amesema siku zote lengo lao ni kuhakikisha wanawahudumia Watanzania wa makundi yote ili kukidhi mahitaji yao ya kujenga kipato imara na uchumi endelevu wa taifa.

“Mwaka huu, Benki ya CRDB tutatoa ‘scholarships’ nne kwa watoto watakaoshiriki matamasha mawili tunayoyadhamini ambayo yanaandaliwa na Kids Holiday Festival yatakayofanyika Dar es Salaam na Moshi katika msimu huu wa sikukuu. Lengo letu ni kuwajengea msingi imara wa masuala ya fedha watoto wetu tangu wakiwa wadogo,” amesema Adili.

Adili amefafanua kwamba ushiriki wa Benki ya CRDB katika matamasha hayo ni mwendelezo wa mkakati wa kuwa jirani na wananchi na matamasha haya yanatoa jukwaa muhimu katika malezi ya watoto kwani huwawezesha wazazi au walezi kutambua vipaji na uwezo wa watoto wao pindi wanapochangamana na wenzao.

Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili (kushoto) akibadilishana nyaraka na Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kids’ Holiday Festival, Geraldine Mashele (kulia) baada ya kusaini mkataba wa ushirikiano wa kuandaa matamasha ya watoto katika hafla iliyofanyika makao makuu ya Benki ya CRDB. Anayeshuhudia ni Meneja Mwandamizi wa Huduma kwa Vijana wa Benki ya CRDB, Mshindo Magimba (katikati).

Licha ya michezo itakayofanyika kwenye matamasha hayo, Adili amesema maafisa wa Benki ya CRDB watatoa elimu ya fedha, ushauri wa huduma za Benki na kufungua akaunti kwa watoto ambao wazazi au walezi wao watapenda kufanya hivyo.

Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kids’ Holiday Festival, Geraldine Mashele amesema huu ni msimu wa pili wa matamasha wanayoyaandaa kwa ajili ya watoto wakitanuka kwenda mikoani.

“Maisha ni fedha hivyo ni muhimu kwa mtoto kuwa na elimu stahiki tangu akiwa mdogo ili aweze kujisimamia pindi atakapokuwa mkubwa. Mwaka jana tulianza kwa tamasha moja lililofanyika hapa Dar es Salaam lakini mwaka huu tumeenda Moshi pia. Tukishirikiana na Benki ya CRDB tutaendelea kutanuka katika mikoa mingi zaidi,” amesema Geraldine.

Ili kuendeleza mkakati wa watoto kupata elimu ya fedha, Geraldine amesema wanakusudia kuanzisha klabu za watoto katika shule mbalimbali ambazo zitakuwa zinatoa fursa kwa watoto kucheza na kujifunza masuala ya fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *