Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wanawake wakilalamikia kukumbwa na vikwazo katika upataji mikopo kupitia majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, Serikali imepanga kushirikiana na asasi za kiraia na wadau wengine wa sekta binafsi kuhakikisha kundi hilo linatimiza vigezo na hatimaye kupata mikopo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima, ukiacha vikundi vinavyopokea mikopo, wapo wengi wanaomtumia ujumbe mfupi kwenye mitandao yake ya kijamii, kumweleza wanakumbwa na vikwazo.
Amesema ameona umuhimu wa kulifikia kundi hilo kwanza, kujua kiini cha vikwazo wanavyokumbana navyo na kama ni vigezo, Serikali ishirikiane na asasi za kiraia na wadau wengine wawasaidie wavitimize na hatimaye wanufaike na mikopo.
Hata hivyo, kinachoelezwa na Dk Gwajima kimetokana na kinacholalamikiwa na baadhi ya wananchi wanaosema mara nyingi wanakwaa kisiki kupata mikopo huku wakirudishwa mara kwa mara hadi wamejenga hisia kuwa inatolewa kwa kuzingatia itikadi ya mtu kisiasa.
Neema Moris Mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam amesema imekuwa vigumu kuifuatilia na kunufaika na mikopo hiyo kwani wamekuwa wakienda kuomba bila mafanikio hadi amekata tamaa.
Mariam Hussein mkazi wa Kimara, Dar es Salaam, amesema mikopo hiyo ameiona inawalenga mabalozi wa nyumba 10 na viongozi wa serikali za mitaa kwa sababu kila akiomba anakosa.
Dk Gwajima ameyasema hayo leo Jumatano Desemba 17, 2025, alipofanya ziara wilayani Ubungo, kuwatembelea wanawake waliokumbwa na vikwazo hivyo, sambamba na walionufaika na mikopo kupitia programu za uwezeshaji wanawake kiuchumi.
Amesema ukiacha vikundi vinavyopata mikopo kupitia programu za uwezeshaji wanawake kiuchumi, lipo kundi kubwa la wanawake walioomba mikopo hiyo bila mafanikio.
Lipo lingine, amesema limeendelea kuomba na kila siku linaambiwa halijatimiza vigezo vya kupata mikopo hiyo, hivyo linaishia kuendelea kuomba muda mwingi.
Amesema makundi hayo ndio ambayo mara nyingi amekuwa akipokea jumbe kupitia simu yake ya mkononi na mitandao yake ya kijamii wakilalamika kunyimwa mikopo hiyo.
Kwa sababu hiyo, Dk Gwajima amesema ameona umuhimu wa kuwafikia wanawake hao ili kujua uhalisia wa sababu za kukosa mikopo hiyo na kutafuta njia za kuhakikisha wanapata.
“Lipo kundi la wanawake linalolalamikia kukosa mikopo hivyo natarajia kuitumia ziara hii kulifikia kundi la walioomba na kukosa, mwisho wa siku tatizo lisiwe kukosa vigezo,” amesema.
Katika kukabiliana na baadhi ya vikundi kukosa mikopo hiyo, amesema tayari ameandaa mkakati wa kushirikiana na sekta binafsi zikiwemo asasi za kiraia kuvisaidia kuikamilisha vigezo stahiki.
Amesema kwa taarifa na ziara yake hiyo, amegundua wengi wanaokosa mikopo hiyo ni kwa sababu hawajatimiza vigezo ikiwemo kushindwa kuandika mapendekezo ya miradi, katiba na wakati mwingine urasimu serikalini.
Ameeleza mkakati anaokuja nao wa kushirikiana na asasi za kiraia kuwasaidia wanaokosa utawawezesha kutimiza vigezo na hatimaye wengi wasikose kwa kushindwa mambo fulani.
“Tunataka tuwafikie ili tujue, kuna shida gani, wanakosa vyeti vya kuzaliwa wanakosaje, wanashindwaje kuandika maandiko ya miradi,” amesema.
Amesisitiza umuhimu wa kubuniwa mikakati ya kuwasaidia ili kuhakikisha wote wanatimiza vigezo na kama changamoto izungumzwe suala la kukosa mikopo na sio kukosa vigezo.
Pia, amewataka viongozi wa Serikali kuhakikisha wanakuwa wawezeshaji badala ya vikwazo vya upatikanaji wa mikopo hiyo kwa wanawake na ile ya makundi mengine.
Kwa upande wake Diwani wa Mbezi, Pius Nyantori amesema anafahamu kuwepo kwa vikundi 16 katika Kata ya Mbezi vilivyopata mikopo na baadhi havikurudisha.
Hata hivyo, amesema kuna taratibu nyingi zimewekwa kwa ajili ya kupata mikopo, ni vema kuziangalia upya ili kuepusha mianya ya rushwa.
Akizungumzia hilo, Dk Gwajima ameeleza hilo pamoja na mengine ndio yaliyosababisha afanye ziara hiyo, akisisitiza kwamba ameelekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kufuatilia hata changamoto za kisera ili zifanyiwe kazi haraka.
Pia, amesisitiza mikopo inayotolewa kupitia majukwaa hayo ni maalumu kwa wananchi wote bila kujali itikadi zao za kisiasa, hivyo viongozi wa chini wasimamie hilo.
Amesema uwezo wa kiuchumi ni muhimu kwa sababu ndio nyenzo hata ya kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake.
Amewasisitiza wanawake wengine kuhakikisha wanajiunga na majukwaa hayo ili wawe wanufaika wa mikopo na hatimaye kujiinua kiuchumi.
“Kuna watu wanadhani majukwaa hayo ni kwa ajili ya watu wa itikadi fulani, sio kweli bali Kila mtu ana fursa ya kuwa sehemu ya majukwaa hayo na hatimaye kuinuliwa,” amesema.
Agnes Mapunda ni mwanakikundi cha Tanzanite kutoka Mbezi Msakuzi, amesema imewachukua mwaka mmoja hadi kupata mkopo.
Ameeleza tatizo lilikuwa kwenye ufuatiliaji uliochukua muda mrefu na walipewa mafunzo ya kuendesha mradi mara nne na wawezeshaji waliwasaidia kufanikisha.
Amesema kinachochelewesha zaidi ni baadhi ya wanakikundi kukosa viambatanishi muhimu kama vyeti vya kuzaliwa au vitambulisho vya Taifa, ambavyo upatikanaji wake una mchakato mrefu.
“Wengine wanashindwa kuanzika mapendekezo ya mradi. Sisi wanakikundi wote ni wasomi hivyo haikutupa ugumu sana kuandika hivyo viambatanisho na hatimaye kupata mkopo na sasa tunafanya mradi wa kufuga kuku,” amesema.