Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi, ametoa tahadhari kwa wamiliki na watumiaji wa Ndege Nyuki (Droni) kufuata sheria ili kulinda usalama wa anga la Tanzania sambamda na kuonya kuwa matumizi yasiyo sahihi yanaweza kuhatarisha usalama wa watu na taifa kwa ujumla.
Msangi amesema kuwa licha ya vifaa hivyo kuwa sehemu ya ubunifu wa kazi unaoongeza fursa za ajira na msaada kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, utalii, ujenzi na tafiti.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa faida hizo zinaweza kupotea endapo matumizi hayatasimamiwa ipasavyo.
“Anga letu ni mali ya taifa na ni wajibu wa kila mtumiaji kulilinda hivyo tusipowajibika kikamilifu hata faida hizo zinaweza kupotea endapo matumizi hayatasimamiwa ipasavyo” alisema Msangi na kuongeza kuwa TCAA ina jukumu la kuhakikisha usalama kwa watumiaji wote wa anga la Tanzania.
“Wamiliki na watumiaji wa ndege nyuki wanapaswa kuchukua hatua za msingi kabla ya kutumia teknolojia hiyo. Kila mtu iwe ni mtu binafsi, kampuni au taasisi anapaswa kuhakikisha droni yake imesajiliwa, amepata mafunzo sahihi na vibali kutoka TCAA.” amesisitiza Msangi
Mbali na wamiliki wa ndani, TCAA imesema watalii na wageni kutoka nje ya nchi wanaruhusiwa kutumia ndege nyuki kwa kufuata taratibu zilizopo.
Imeandaliwa na @moseskwindi