‘Mchezo mchafu’ usafiri wa mabasi usifumbiwe macho‘Mchezo mchafu’ usafiri wa mabasi usifumbiwe macho

KATIKA kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, kumekuwapo na ongezeko kubwa la wasafiri wa masafa marefu, hasa kwa mabasi wakienda kusherehekea sikukuu za Krisimasi na Mwaka Mpya.

Ni kipindi ambacho mahitaji ya vyombo vya usafiri huongezeka kiasi cha mamlaka kutoa usajili wa muda wa vibali vya usafirishaji kwa watu wanaotaka kufanya hivyo kwa kuweka vigezo.

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) huchukua hatua za kutoa leseni za muda mfupi kwa mabasi ili kuongeza huduma katika njia zenye mahitaji makubwa kipindi cha sikukuu na kupunguza msongamano wa usafiri.

Vilevile, hiki ni kipindi ambacho huwapo changamoto ambazo hurudisha nyuma jitihada za kuboresha usafiri nchini. Moja ya changamoto hizo ni ulanguzi wa tiketi, matapeli na biashara haramu ya tiketi, ambayo husababisha wasafiri kushindwa kupata huduma kwa haki na wakati muafaka.

Mathalani, katika gazeti hili jana kulikuwa na habari kuhusu wakala wa basi la kampuni moja anayetafutwa na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani wilayani Kahama akituhumiwa kumtoza abiria Sh 135,000 kinyume cha sheria.

Aidha, inapofika tarehe za karibu na Krisimasi, vitendo vya ulanguzi wa tiketi katika Kituo cha mabasi cha Magufuli Dar es Salaam, huripotiwa wakidaiwa kuuza tiketi za karatasi kwa gharama kubwa kwa wasafiri wanaokwenda mikoa mbalimbali.

Huu ni mchezo mchafu ambao watu wasio waaminifu hukandamiza haki za wasafiri na wakati huo huo kuipotezea serikali mapato.

Hata hivyo, tunapongeza mamlaka mbalimbali za serikali ambavyo hufanya kazi ya ziada kusimamia usafirishaji huu wa umma katika kipindi hiki cha sikukuu.

Rai yetu kwa serikali ni kuongeza jitihada za kusimamia mfumo wa tiketi mtandao unaolenga kuhakikisha tiketi zinapatikana kwa njia rasmi na salama.

Mfumo huu wa mtandao unatoa uwazi zaidi, unafanya taarifa za wasafiri kuwa rahisi, na hupunguza fursa za ulanguzi na ulaghai unaohusiana na tiketi za mabasi.

Kwa upande wa wasafiri, wanapaswa kuelewa kuwa kununua tiketi kwa njia rasmi kunawalinda dhidi ya udanganyifu wa tiketi za karatasi zinazouzwa kwa bei ya juu na wakati mwingine zinaweza kuwa bandia.

Wananchi hawana budi kutambua kwamba tiketi za mtandaoni ni muarobaini wa utapeli na matapeli.

Ni matumaini yetu kwamba serikali itaendeleza mikakati ya kudhibiti ‘mchezo mchafu’ katika usafiri wa mabasi kwa kushirikisha wadau mbalimbali na zaidi kwa kuendelea kuelimisha wananchi juu ya mifumo ya tiketi mtandao.

Wakati huo huo, wananchi na wasafiri wanapaswa kushirikiana kikamilifu na juhudi hizi za serikali kwa kununua tiketi kwa njia rasmi na kutumia teknolojia inayoelekeza matumizi ya mtandao badala ya kutegemea wapigadebe wasio waaminifu.

Kwa kufanya hivyo, usalama wa usafiri utaongezeka, udanganyifu utapungua kama si kukoma na kuhakikisha kila
msafiri anapata huduma bora na salama, hasa wakati huu wimbi la wasafiri kuelekea sikukuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *