
DIRISHA dogo la usajili lipo njiani kufunguliwa mapema mwakni, huku Yanga ikiwa haijakaa kinyonge ikipanga kuongeza mashine moja ya maana eneo la ushambuliaji na hivi unavyosoma tayari kuna majina manne mezani kwa mabosi wa klabu hiyo wakipiga hesabu waondoke na nani kati yao.
Kocha timu hiyo, Pedro Goncalves ameutaka uongozi kumletea mashine hiyo ya kuongeza nguvu eneo hilo ambalo kwa sasa linamtegemea zaidi Prince Dube kutokana na Clement Mzize kuwa majeruhi huku, Andy Boyeli aliyetua kwa mkopo kutoka Afrika Kusini akiwahindwa kufanya maajabu.
Taarifa zilizopenyezwa kwa Mwanaspoti ni kwamba mezani kwa mabosi wa Yanga kuna majina manne, akiwamo Muangola Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Depu’ ambaye tuliwadokeza wiki iliyopita sambamba na nyota kutoka Cameroon anayekipiga kwa sasa Stade Malieni, Taddeus Nkeng.
Pia kuna majina mengine mawili ya washambuliaji wanaojadiliwa na mabosi wa Yanga kutoka Ivory Coast na DR Congo yaliyofanywa siri, ambao sambamba na wenzao watasubiri uamuzi wa kocha Pedro aliyeachiwa msala wa kuamua mmojawao aje kuungana na kina Dube na Mzize, wakati Boyeli akipigiwa hesabu za kurudishwa Sekhukhune ya Afrika Kusini.
Ipo hivi. Licha ya kusajiliwa kwa mbwembwe kutokana na rekodi tamu alizokuna nazo kabla ya kutua nchini kuanzia kule Zambia alikokuwa akiitumikia Power Dynamos kisha Sekhukhune United, Yanga ilimbeba Boyeli, lakini mambo yamembadilikia akiwa amefunga mabao mawili tu ya Ligi hadi sasa.
Kiwango hicho cha Boyeli kimeonekana kutowaridhisha mabosi wa klabu hiyo, lakini kimemfanya pia akose nafasi ya kucheza muda mwingi, hivyo wanapiga hesabu za kumrudisha Sauzi mapema, huku Prince Dube ambaye mkataba wake upo ukingonui akihakikishiwa maisha ya kocha Pedro.
Lakini, kocha huyo ameagiza aletewe straika mmoja wa maana na tayari yanga imeanza kuwasiliana na wachezaji wanne tofauti akiwamo straika wa Stade Malien iliyotoka kuifunga Simba mabao 2-1 katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika aitwae Taddeus Keng mwenye urmi wa miaka 25.
“Yanga imewasiliana na Stade Malien kuangalia uwezekano wa kumpata mshambuliaji Taddeus. Malien hawajawawekea ugumu Yanga na tayari wameshawatajia bei yake na changamoto pekee ambayo itakutana nayo ni jamaa amecheza michuano ya Ligi ya Mabingwa na wao wanataka mshambuliaji atakayecheza mashindano hayo,” kilisema chanzo kutoka ndani ya Yanga na kuongeza;
“Jina la Nkeng na jamaa wengine watatu yameshawasilishwa kwa kocha Pedro na siku yoyote kuanzia Leo ili wachague mmoja kwani kuna mshambuliaji wa Ivory Coast na mwingine Kongo, ambayo majina yao hayajawekwa wazi bado.”
Jina jingine ni kama lile ambalo Mwanaspoti lilifichua wiki iliyopita ambalo ni la Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Depu’ anayejulikana kwa kiwango chake bora, ukiachilia mbali vigezo vinavyombeba.
Depu anaichezea Radomiak Radom ya Poland akitokea Vojvodina ya Serbia ambayo alichezea kiungo wa Simba, Morice Abraham msimu uliopita, akifunga mabao manane.
Akizungumza na Mwanaspoti, beki wa zamani wa Yanga, Joyce Lomalisa Mutambala anayeitumikia Sagrada Esperanca ya Angola alimchambua Depu kwa kusema ni mmoja kati ya washambuliaji bora.
“Namjua tangu alipoanza kucheza soka la ushindani ni mshambuliaji mzuri kama Yanga wakimpata watakuwa wamepata chombo kweli,” alisema Lomalisa na kuongeza;
“Anajua kufunga, ana nguvu na akili ya kupambana na mabeki. Kama akipatikana anaweza kuwa mshambuliaji aliyekaribia makali ya Fiston Mayele.”
MZIZE BADO
Mwanaspoti ilidokeza wikiendi juu ya Mzize, straika na kinara wa mabao wa msimu uliopita wa klabu kuzua presha mpya ndani ya Yanga, baada ya ripoti ya madaktari wa kikosi hicho kuwafikia mabosi kuwa mshambuliaji huyo hatarejea kwa haraka hadi apone kabisa.
Makadirio ya Mzize kurejea ni kati ya Februari mwakani, hivyo Yanga itamkosa mshambuliaji huyo katika mechi zote za makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, timu hiyo ikiwa Kundi B sambamba na Al Ahly ya Misri, AS Far Rabat ya Morocco na JS Kablyie ya Algeria.
Straika huyo aliyemaliza msimu wa ligi iliyopita akiwa na mabao 14 akishika nafasi ya pili nyuma ya Jean Charles Ahoua wa Simba aliyekuwa na mabao 16 akiwa ndiye kinara wa Ligi Kuu, tayari ameanza mazoezi mepesi, lakini ripoti ya madaktari atarudi uwanjani akiwa kamili pengine Februari mwakani.