
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema ushirikiano wa kimkakati kati ya Iran na Russia umeingia “hatua mpya na ya kasi zaidi” kufuatia kutiwa saini kwa ramani ya ushirikiano ya miaka mitatu pamoja na mwenzake wa Russia, Sergei Lavrov.
Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Moscow Jumatano, Araghchi alithibitisha kuwa hati hiyo mpya inaweka ajenda ya wizara za mambo ya nje za nchi hizo mbili kwa kipindi cha 2026 hadi 2028, ikiwa kama “ramani ya ushirikiano wa miaka mitatu ijayo.”
Amesema: “Leo tumefanya mazungumzo ya karibu, ya kina na ya undani katika maeneo yote, ya pande mbili, ya kikanda na ya kimataifa.”
Waziri huyo alibainisha kuwa uhusiano wa pande mbili umepanuka kwa kiwango kikubwa, hasa mwaka huu, na kupata msukumo mpya kupitia utekelezaji wa mkataba wa ushirikiano wa kimkakati kati ya mataifa hayo mawili.
Araghchi amesisitiza uimara wa mahusiano ya kisiasa, akionyesha kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu cha serikali ya sasa, marais wa Iran na Russia wamekutana mara tano. Mkutano wa hivi karibuni ulifanyika Desemba 12 mjini Ashgabat, Turkmenistan, ukiashiria mwendelezo wa mawasiliano ya ngazi ya juu.
Alisema uhusiano kati ya nchi hizo mbili “unapanuka kwa kiasi kikubwa” katika sekta ya uchumi.
Aidha, alitaja maendeleo makubwa katika sekta muhimu kama nishati, usafiri na usafirishaji, akisisitiza umuhimu wa mradi wa kimkakati wa Korida ya Kaskazini-Kusini na sehemu muhimu ya reli ya Rasht–Astara.
Araghchi amesema biashara ya pande mbili inaendelea kupanda, huku njia mpya za ushirikiano zikiendelezwa. Ameongeza kuwa kamati ya pamoja ya kiuchumi yenye makundi 17 maalumu ya kazi inatarajiwa kukutana Februari.
Akizungumzia msimamo wa nyuklia wa Iran, Araghchi amesisitiza haki za kisheria za Iran chini ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).
Amesema: “Iran, kama mwanachama mwaminifu wa NPT, inatekeleza wajibu wake wote, lakini haitawahi kuachana na haki zake za kisheria chini ya mkataba huo.”
Amesema matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia, ikiwemo urutubishaji madini ya urani, ni “haki isiyopingika” ya Iran.
Araghchi amelaani mashambulizi ya siku 12 yaliyofanywa na Marekani na Israel dhidi ya Iran mwezi Juni, na akashukuru Russia kwa kusimama na Iran na kulaani mashambulizi hayo yasiyo halali.
Amebaini kuwa: “Shambulio la Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, licha ya kuharibu baadhi ya majengo na vifaa, halikuweza kuangamiza teknolojia ya ndani ya nchi wala kudhoofisha azma ya Iran.”
Katika uwanja wa kimataifa, Araghchi amesema kuna “muwafaka wa wazi wa mitazamo” kati ya Iran na Russia katika kukabiliana na mfumo wa ubabe, vitisho na undumakuwili wa mataifa ya Magharibi, hususan Marekani.
Ameongeza kuwa Iran na Russia zinashirikiana kwa karibu katika kukabiliana na vikwazo visivyo halali na hatua za upande mmoja, na kwamba ushirikiano wao unaimarika ndani ya taasisi za kikanda na kimataifa kama BRICS, Jumuiya ya Ushirikino ya Shanghai (SCO) na Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia.