Mtafiti mmoja kutoka Iran ametwaa medali ya dhahabu katika Tamasha la Kimataifa la Uvumbuzi la Silicon Valley (SVIIF) 2025 huko California, Marekani kufuatia utengenezaji wa dawa bunifu inayochangia katika matibabu ya saratani.

Kwa mujibu wa IRNA, Dkt. Maryam Nouri Balanji alipata tuzo kuu ya heshima katika hafla hiyo maarufu baada ya kubuni dawa ya kisasa ya recombinant, inayotokana na misombo ya sukari iliyochujwa kutoka kwa Holothuria scabra, aina adimu ya majongoo wa baharini wanaopatikana katika maji ya kaskazini mwa Kisiwa cha Qeshm, Iran.

Uvumbuzi huo, uliokusudiwa kwa matumizi ya kitabibu kwa binadamu, unaweza kutengenezwa katika mfumo wa sindano au tembe, na umeundwa kuzuia ukuaji wa seli za saratani pamoja na kuangamiza uvimbe wa aina mbalimbali.

Mradi huo uliendelezwa na Dkt. Balanji kwa ushirikiano na wataalamu wenzake kutoka Baraza Kuu la Maeneo Huru ya Kiuchumi, pamoja na timu ya wabobezi kutoka Kanada.

Uvumbuzi huo uliibuka mshindi wa kwanza duniani katika SVIIF 2025, na kila mwanachama wa timu ya utafiti akatunukiwa medali ya dhahabu.

Hii ni mara ya pili kwa mtafiti kutoka maeneo huru ya kiuchumi ya Iran kupata heshima ya kiwango hiki katika majukwaa ya kimataifa.

Dkt. Balanji hapo awali alishinda nafasi ya kwanza na medali ya dhahabu katika Tamasha la Uvumbuzi na Ubunifu la Kaohsiung 2023 nchini Taiwan, lililoandaliwa chini ya Chama cha Wamiliki wa Haki za Uvumbuzi Duniani (WIPA), ambako pia alikabidhiwa ufadhili kamili wa masomo kutoka Finland.

SVIIF 2025, linaloandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Wavumbuzi (IFIA), linatambulika kama moja ya matukio makubwa zaidi duniani ya ubunifu. Tamasha hilo lilifanyika kuanzia Agosti 8 hadi 10 katika Kituo cha Mikutano cha Santa Clara, California, na likawakutanisha wavumbuzi na wabunifu kutoka pembe zote za dunia.

Washiriki walionesha uvumbuzi na teknolojia mbalimbali za kisasa katika nyanja za afya na tiba, nishati safi, ulinzi wa mazingira, shughuli za upyaishaji nishati, kilimo mahiri, na sekta ya chakula.

Mbali na kuwasilisha ubunifu mpya katika jukwaa la kimataifa, tamasha hili pia hutumika kama kitovu cha mtandao wa ushirikiano wa kimataifa, kibiashara na kiwanda, miongoni mwa washiriki kutoka mataifa mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *