Kituo kimoja nchini Afrika Kusini kinachoshughulikia maombi ya visa za Marekani kimevamiwa na maafisa wa uhamiaji wa Afrika Kusini na kuwatia mbaroni raia saba wa Kenya waliokuwa wanafanya kazi nchini humo kinyume cha sheria.

Kituo hicho cha Johannesburg kilikuwa kinashughulikia maombi ya Waafrikana chini ya mpango wa utawala wa Trump wa kuwapa ukimbizi makaburu kwa madai kuwa wananyanyaswa nchini Afrika Kusini.

Wakenya hao walikuwa wakifanya kazi katika kituo hicho pamoja na maafisa wa Marekani licha ya kuingia Afrika Kusini kwa visa vya utalii. Mtu anayeingia kwa visa ya utalii haruhusiwi kufanya kazi nchini Afrika Kusini.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afrika Kusini ilisema jana kwamba, hakuna maafisa wa Marekani waliokamatwa katika uvamizi huo wa siku ya Jumanne na kwamba eneo hilo halikuwa la kidiplomasia.

Uvamizi huo utaongeza mvutano kati ya Marekani na Afrika Kusini. Katika kuendeleza chuki zake dhidi ya wageni na hasa Waafrika, Donald Trump – rais wa Marekani – amedai kuwa nchi hiyo imeamua kuwapa ukimbizi makaburu wa Kiafrikana wa Afrika Kusini kwa kile anachodai kuwa Pretoria inawanyanyasa wazungu hao. Madai ya Trump yanaendelea kupingwa hadi hivi sasa na yanahesabiwa ni uchochezi wa wazi wa kikabila tena kwenye nchi ambayo Marekani haihusiki nayo kivyovyote vile.

Serikali ya Afrika Kusini imesema kwamba Waafrika Kusini weupe hawajatimiza vigezo vya kuwa wakimbizi kwa sababu hakuna mateso wanayofanyiwa huko Afrika Kusini ingawa pia imesema, kila raia wa Afrika Kusini yuko huru kuishi mahala popote anapotaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *