KUNA maswali mengi yameibuka baada ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Desemba 15, 2025 ilipopitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya uamuzi uliopokewa kwa mitazamo tofauti.

Miongoni mwa maswali yaliyoibuka ni kutokana na adhabu za kuwafungia wachezaji mechi tano kwa makosa ya vitendo visivyo vya kiuanamichezo. Pia kwa kosa la shabiki kuruka uzio na kuingia katika eneo la kuchezea (pitch) aliyeonekana kufika hadi kwenye goli la timu ya Coastal Union na kuinama kama ishara ya kutafuta, kuchukua ama kuweka kitu.

Muda mfupi baada ya Desemba 16, 2025 Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kutoa taarifa ya uamuzi uliofanywa katika kikao hicho cha kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, maoni mengi yaliyowasilishwa ni kutokubaliana na hilo.

Mmoja kati ya waliotoa maoni hayo, amesema: “Hizi kamati sasa zimekuja kuua viwango vya wachezaji, kumfungia mchezaji mechi tano ni kuua kiwango chake, kazi inatakiwa kuonya na kulinda maslahi ya wachezaji wote, kutetea mmoja na kuua kiwango cha mwingine haileti mantiki.”

Mwingine aliongeza: “Mechi tano ni nyingi sana jamaa! Kama kadi nyekundu tu ambayo ipo kikanuni ni mechi tatu, iweje kamati itoe mechi tano? Vipi kuhusu kiwango cha mchezaji?”

Pia yupo aliyesema: “Kiukweli adhabu ya Yanga inachekesha sana. Kwa kigezo gani hiyo adhabu imetoka, je ikiwa alikuwa shabiki wa timu nyingine akaamua kuvaa jezi ya Yanga na kwenda kutekeleza hilo tukio?”

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah, alisema: “Kwanza hizi adhabu za wachezaji zinatolewa kama kubalansi, mfano ikitokea mchezaji wa Yanga akiadhibiwa basi na wa Simba naye ionekane ameadhibiwa, kwa sababu baada ya lile tukio la Bacca (Ibrahim Abdullah wa Yanga) ambalo kisheria hakutakiwa aadhibiwe na kamati kwa sababu limetokea mchezo unaendelea na refarii hakupuliza filimbi. Kwa hiyo hakutakiwa aadhibiwe, ilitakiwa refarii kubeba jukumu hilo.

“Kwa kawaida refarii akiwa hajaona tukio, anatakiwa kabla ya kuandika ripoti aangalie marudio ya baadhi ya matukio ili aandike ripoti kuonyesha kuna tukio lilitokea na hakuwa ameliona. Naona kamati inafanya uamuzi ambao ulipaswa kufanywa na refa kitu ambacho ni kibaya sana kwa mpira.

“Sasa hapa hatujafikia mwisho wa duru la kwanza, kuna watu watano wameadhibiwa mechi tano tano, tutakapokuwa tunamaliza itakuwaje. Tukiendelea hivi tutafika kubaya.

Kuhusu tukio la shabiki kuingia uwanjani iliyofanya Yanga kuadhibiwa, Angetile alisema: “Mimi najua klabu inaadhibiwa pale mashabiki wengi wanapofanya vurugu na kwa sababu uwanjani huwa kumepangwa mwenyeji na mgeni, kwa hiyo inajulikana kabisa mashabiki wa timu fulani wapo upande huu, lakini hili la shabiki mmojammoja ni kama wamechemka.

“Haiwezekani shabiki mmoja akafanya fujo ukaenda kuiadhibu klabu, ni yeye mwenyewe. Kama kumfungia iwe asiingie uwanjani tena anapelekwa kamati ya nidhamu na sio ile kamati iliyofanya uamuzi.

“Haya matukio mengine kama shabiki kuingia uwanjani inatakiwa kamati ya nidhamu kuamua, sio Kamati ya Ligi. Lakini kama hujamuita na unasema huyu ni shabiki wa Yanga, hapo hakuna haki.”

Katika taarifa juu ya adhabu hiyo Bodi ya Ligi ilisema, Yanga imetozwa faini kwa mujibu wa Kanuni 47:1 ya Udhibiti wa Klabu kwa shabiki huyo waliyemnasibisha na Yanga kwamba aliruka ukuta na kuwapita walinzi kuingia uwanjani akienda eneo la lango la Coastal Union waliokuwa wenyeji na kuinama kama anayetafuta kitu au kuweka au kutoa kitu, huku ikisisitiza klabu kuwaelimisha wachezaji, viongozi na mashabiki juu ya uungwana mchezoni na kuepuka kulitia aibu soka.

ADHABU ZENYEWE

Kiungo wa Singida Black Stars, Khalid Aucho amefungiwa mechi tano na kutozwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kufanya kitendo kisicho cha kiuanamichezo kwa kumpiga na kumsukuma mshambuliaji wa TRA United, Adam Adam wakati timu hizo zilipokutana Desemba 6, 2025 huku mwamuzi wa kati wa mechi hiyo, Alex Pancras akipewa onyo kali kwa kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kutochukua hatua stahiki kwa kitendo hicho.

Pia mshambuliaji wa Simba, Jonathan Sowah na kiungo wa timu hiyo, Allasane Kante, wamefungiwa kucheza mechi tano kila mmoja kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu waliyofanya dhidi ya wachezaji wa Azam, timu hizo zilipokutana Desemba 7, 2025.

Sowah alifanya kitendo kisicho cha kiuanamichezo kwa kumpiga kiwiko Himid Mao, huku Kante akimpiga teke kwa makusudi Feisal Salum. Mbali na kufungiwa, wachezaji hao kila mmoja ametozwa faini ya Sh1 milioni.

Mwamuzi wa kati wa mechi hiyo, Abdallah Mwinyimkuu ameondolewa kuchezesha katika mizunguko mitano ya Ligi Kuu kwa kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua kwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria za mpira vilivyofanywa na wachezaji hao.

Kwa upande wa Yanga, imetozwa faini ya Sh5 milioni kwa kosa la shabiki wake kuruka uzio na kuingia kwenye eneo la kuchezea (pitch) wakati timu hiyo ikiwa ugenini dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma, Desemba 7, 2025 ambapo shabiki huyo alionekana kufika hadi kwenye goli la Coastal Union na kuinama kama ishara ya kutafuta, kuchukua ama kuweka kitu.

Tukio kama hilo linafanana na lile lililotokea Machi 15, 2024 ambapo shabiki wa Simba aliyetambuliwa kwa jina la Mohamed Salehe, alikuja kufungiwa kutohudhuria mechi yoyote kwa muda wa mwaka mmoja, kwa kosa la kuingia uwanjani wakati mechi ya Ligi Kuu kati ya timu hiyo dhidi ya Mashujaa FC ikichezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar.

Pamoja na hilo, Simba ilipigwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la walinzi wake na shabiki kupanga njama na kufanikisha azma ya kuingia uwanjani na kufanya vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina.

Taarifa ilieleza, shabiki huyo alionekana kupitia video fupi iliyosambaa mitandaoni na walijadiliana na mlinzi wa uwanjani kabla ya kuingia na kufanya tukio hilo lililoleta taswira mbaya kwa Ligi ya Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *