Chanzo cha picha, Moose Campbell/BBC
-
- Author, Jonathan Beale
- Nafasi, Defence correspondent in Kyiv
-
Muda wa kusoma: Dakika 5
Tunasafirishwa tukiwa tumefungwa macho kuelekea eneo la siri ambako Ukraine inatengeneza moja ya silaha zake za kisasa zaidi. Tunatakiwa kuzima simu zetu kabisa, kiwango cha usiri kinachozunguka uzalishaji wa kombora la masafa marefu la Flamingo ni kikubwa sana.
Kwa Ukraine, kusambaza na kuficha uzalishaji wa silaha kama hizi ni suala la kufa au kupona. Kuna viwanda viwili kama hivi vimewahi kushambuliwa.
Ndani ya kiwanda tunachotembelea, tunaonywa tusipige picha kuonyesha miundombinu kama nguzo, madirisha au dari. Pia tunaombwa tusionyeshe nyuso za wafanyakazi wanaohusika kutengeneza silaha, ambako makombora ya Flamingo yako katika hatua mbalimbali za kukamilishwa.
Licha ya mashambulizi yanayoendelea, Ukraine inaongeza kasi ya sekta yake ya uzalishaji wa silaha. Rais Volodymyr Zelensky anasema nchi hiyo sasa inazalisha zaidi ya asilimia 50 ya silaha zote zinazotumika vitani. Takribani silaha zake zote za masafa marefu zinatengenezwa ndani ya nchi.
Mwanzoni mwa vita, Ukraine ilitegemea zaidi silaha zake za zamani za enzi ya Umoja wa Kisovieti. Msaada wa kijeshi kutoka Magharibi uliisaidia kuimarisha jeshi lake, lakini sasa Ukraine inaongoza duniani katika maendeleo ya mifumo isiyo na rubani kama roboti na droni.
Na sasa, makombora ya masafa marefu yanayotengenezwa ndani ya nchi yanaongeza uwezo wa Ukraine wa kushambulia maeneo ya mbali.
Chanzo cha picha, Moose Campbell/BBC
Iryna Terekh ni Afisa Mkuu wa Kiufundi wa Fire Point, moja ya kampuni kubwa zaidi za Ukraine zinazotengeneza droni na makombora. Kauli mbiu ya kampuni hiyo kwa Kilatini inatafsiriwa kuwa “kama si sisi, nani mwingine?”
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 33 aliwahi kusomea usanifu majengo, lakini sasa anajitahidi kusaidia kuivunja ngome ya vita ya Urusi.
Anaonekana mdogo mbele ya kombora kubwa la Flamingo, ambalo anasema limepakwa rangi nyeusi badala ya waridi (tofauti na mifano ya awali) “kwa sababu linakunywa mafuta ya Urusi”.
Muonekano wa mwisho wa kombora hilo unafanana na roketi ya Kijerumani ya V1 iliyotumika katika vita kuu ya pili ya dunia. Lina injini kubwa ya ndege juu ya bomba refu lenye urefu sawa na basi moja kubwa.
Makombora haya tayari yametumika vitani, ingawa kampuni hiyo haitaki kuthibitisha ni maeneo gani imeshambulia
Chanzo cha picha, Moose Campbell/BBC
Flamingo ni aina ya silaha ya mashambulizi ya mbali ambayo mataifa ya Magharibi yamesita kuipatia Ukraine.
Kombora hilo la masafa marefu linadaiwa kuwa na uwezo wa kufika kilomita 3,000, sawa na kombora la Marekani la Tomahawk, silaha ya kisasa na ya gharama kubwa zaidi ambayo Rais wa Marekani Donald Trump alikataa kuipatia Ukraine.
Mashambulizi ya mbali yanaonekana kuwa sehemu muhimu ya vita, ambako Ukraine kwa kiasi kikubwa imekuwa ikitumia droni za masafa marefu. Hata hivyo, bado Ukraine inapoteza maeneo kwa Urusi kwenye mstari wa mbele wa mapambano unaoenea kwa zaidi ya kilomita elfu moja. Ndiyo maana Ukraine inazidi kulenga uchumi wa vita wa Urusi, ili kupunguza kasi ya mashambulizi yake.
Mkuu wa Majeshi ya Ukraine, Jenerali Oleksandr Syrskyi, anasema mashambulizi ya masafa marefu ya Ukraine tayari yameigharimu uchumi wa Urusi zaidi ya dola bilioni 21.5 mwaka huu.
Chanzo cha picha, Moose Campbell/BBC
Ruslan, afisa wa Kikosi Maalum cha Operesheni cha Ukraine, anasema mkakati ni rahisi: “Ni kupunguza uwezo wa kijeshi wa adui na nguvu yake ya kiuchumi.”
Anasema vikosi maalum vya Ukraine vimefanya mamia ya mashambulizi dhidi ya viwanda vya kusafisha mafuta, viwanda vya silaha na maghala ya risasi ndani kabisa ya eneo la adui (Urusi).
Bila shaka, Urusi imekuwa ikifanya mashambulizi kama hayo kwa kiwango kikubwa zaidi. Kwa wastani, imekuwa ikirusha takribani ndege zisizo na rubani (droni) 200 za Shahed kwa siku, huku majibu ya Ukraine yakiwa karibu nusu ya idadi hiyo.
Urusi haijielekezi kushambulia maeneo ya kijeshi pekee. Mashambulizi yake ya makombora na droni yamesababisha katizo kubwa la umeme kote nchini Ukraine, na kufanya maisha kuwa magumu kwa mamilioni ya raia.
“Ningependa kurusha droni nyingi kama Urusi,” anasema Ruslan, “lakini tunaongeza uzalishaji kwa kasi kubwa.”
Bi Terekh wa Fire Point anasema Ukraine huenda isiweze kuwa sawa kwa uwezo wa rasilimali kama Urusi, lakini anaongeza: “Tunajaribu kupigana kwa kutumia akili na mbinu.”
Denys Shtilerman, mbunifu mkuu na mwanzilishi mwenza wa kampuni hiyo, anakiri kuwa hakuna “Wunderwaffe” yaani silaha ya miujiza. “Kinachobadilisha mchezo ni nia yetu ya kushinda,” anasema.
Chanzo cha picha, Kevin McGregor/BBC
Fire Point haikuwepo kabisa kabla ya uvamizi kamili wa Urusi wa mwaka 2012. Lakini sasa kampuni hiyo changa inazalisha droni 200 kwa siku. Droni zake aina ya FP1 na FP2, kila moja ikiwa na ukubwa wa ndege ndogo, zimehusika katika asilimia 60 ya mashambulizi ya masafa marefu ya Ukraine. Kila droni hugharimu takribani dola 50,000, ambatyo ni nafuu sana, mara tatu chini ya gharama ya droni ya Urusi aina ya Shahed. Urusi bado inazalisha karibu droni 3,000 kwa mwezi.
Ukraine bado inahitaji msaada wa nje, hasa katika masuala ya kijasusi na fedha. Lakini inajitahidi kuwa huru zaidi. Bi Terekh anasema wameamua kwa makusudi kupata vipuri vingi iwezekanavyo kutoka ndani ya Ukraine.
“Tunaifuata kanuni kwamba hakuna mtu anayeweza kuathiri silaha tunazotengeneza,” anasema. Wanaepuka vipuri kutoka nchi mbili mahsusi, China na Marekani.
Alipoulizwa kwa nini wasitumie vipuri vya Marekani, anasema:
“Tuko kwenye msukosuko wa kihisia na Marekani. Kesho mtu huyu anaweza kuamua kusitisha msaada, na sisi tusipate uwezo wa kutumia silaha zetu wenyewe.”
Hadi mwisho wa mwaka jana, chini ya Rais Joe Biden, Marekani ilikuwa imetoa karibu dola bilioni 70 za msaada wa kijeshi kwa Ukraine. Hilo lilikoma chini ya Rais Trump, ambaye badala yake ameanzisha mpango wa kuruhusu mataifa ya Ulaya ya NATO kununua silaha za Marekani.
Marekani sasa si mfadhili mkubwa zaidi wa kijeshi wa Ukraine, na Ulaya imekuwa ikihangaika kujaza pengo hilo.
Hofu kuhusu msaada wa baadaye wa Marekani imeathiri pia mjadala wa dhamana za kiusalama suala muhimu katika mazungumzo ya sasa ya amani. Bi Terekh anapuuza mazungumzo hayo akiyaita “mazungumzo ya kujisalimisha”, na anasema kuwa kutengeneza silaha zake yenyewe ndiyo njia pekee ya Ukraine kujihakikishia usalama.
Mwanafunzi huyo wa zamani wa usanifu majengo pia anatumai kuwa mataifa mengine ya Ulaya yanaweza kujifunza.
“Sisi ni mfano wa damu,” anasema, “katika suala la kujiandaa kwa vita.”
Anaamini kuwa kama nchi nyingine yoyote ingeathiriwa kwa kiwango ambacho Ukraine imekumbana nacho, “basi tayari ingekuwa imeshatekwa.”