Manchester, England. Meneja wa Manchester City, Pep Guardiola, amewataja nyota wake wawili, Rayan Cherki na Savinho, akisema hawakutimiza wajibu wao wa kiulinzi licha ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Brentford katika Kombe la Carabao na kufuzu nusu fainali.

Mabao ya Cherki na Savinho yaliipa City ushindi huo katika Uwanja wa Etihad, matokeo yanayowaweka vigogo hao wa England kwenye mkondo wa kukutana na mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Newcastle United, katika hatua ya nusu fainali itakayochezwa kwa mechi mbili.

Guardiola alifanya mabadiliko kadhaa kwenye kikosi chake, akiwapumzisha nyota wake muhimu kama Erling Haaland, Gianluigi Donnarumma na Ruben Dias, akijiandaa kwa mchezo muhimu wa Ligi Kuu dhidi ya West Ham Jumamosi.

Baada ya Phil Foden kuingia kuchukua nafasi ya Oscar Bobb aliyeumia mapema, Guardiola alilazimika kufanya mabadiliko manne kipindi cha pili, akilenga kuilinda City na kuongeza kasi ya mchezo.

Akieleza sababu za mabadiliko hayo baada ya mechi, Guardiola amewakosoa wafungaji wake kwa kushindwa kutekeleza majukumu ya kiulinzi.

“Nilifurahi sana na mchango wa wachezaji waliotoka benchi. Kwa sababu kipindi cha pili, Rayan Cherki hakufanya kazi aliyopaswa kufanya kiulinz hakuwa na nguvu. Savinho pia hakuwa na nguvu.

“Ndiyo maana mchango wa Josko Gvardiol, Matheus Nunes, hasa Bernardo Silva, ulisaidia sana kuongeza kasi ya mchezo,” amesema Guardiola.

Guardiola amesema hakutaka kuwatumia Nico Gonzalez na Nico O’Reilly kwa dakika zote 90, kutokana na mzigo wa mechi walizocheza, huku akisisitiza umuhimu wa pambano lijalo dhidi ya West Ham.

“Hali ilikuwa hivyo pia kwa Phil Foden. Sikupenda acheze dakika nyingi alizocheza, lakini jeraha la Oscar Bobb lilitokea. Hata hivyo, kila mchezaji aliyeingia kutoka benchi alifanya kazi kubwa,” amesema.

Licha ya kumkosoa Cherki kwa upande wa ulinzi, Guardiola hakuwa na maneno mabaya kuhusu bao lake la kwanza, lililoipa City uongozi.

Mchezaji huyo aliyesajiliwa kwa pauni 31 milioni majira ya joto aliudhibiti vyema mpira nje ya eneo la hatari na kupiga shuti la mbali lililomshinda kipa Hakon Valdimarsson dakika chache baada ya nusu saa ya mchezo.

Alipoulizwa kufafanua zaidi, Guardiola amesema: “Hata mtu kipofu anaweza kugundua lilikuwa bao la kipekee. Huhitaji kuwa kocha kuelewa ubora wa bao hilo.

“baada ya hapo hakuucheza mchezo vizuri, lakini kabla na wakati wa bao, alikuwa bora sana,” amesema Guardiola.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *