l

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Ian Williams
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Frank Onyeka amemuelezea Victor Osimhen “kuwa yuko katika kiwango kikubwa” na anaamini mabeki wa upinzani katika Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) la 2025 “wanamwogopa” mshambuliaji huyo wa Nigeria.

Onyeka na Osimhen ni sehemu ya kikosi cha Super Eagles kilichopangwa kusaka ushindi baada ya kushindwa katika fainali ya Afcon ya 2023 na wenyeji Ivory Coast, mchezo ambao wachezaji wote wawili walianza.

Osimhen, mwenye umri wa miaka 26, alipata bao mara moja tu wakati wa mashindano hayo, lakini sasa anashika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji mabao wa muda wote wa Nigeria akiwa na mabao 31 katika mechi 45, nyuma ya Rashidi Yekini.

“Ni mchezaji mzuri sana,” Onyeka aliambia BBC Sport Africa.

“Ni mtu anayetaka kucheza kila mpira. Kwangu mimi, nadhani mabeki wanamuogopa. Victor yuko katika kiwango kingine.”

Super Eagles walipata pointi nne pekee kati ya pointi 15 wakati Osimhen alipokosekana wakati wa mechi zao ya kufuzu Kombe la Dunia la 2026 na haikufanikiwa kufuzu.

Na timu hiyo pia ilionekana kupoteza mwelekeo katika mechi yao ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya DR Congo wakati mchezaji huyo wa Galatasaray alipotolewa wakati wa mapumziko.

“Kumkosa Victor kuelekea kipindi cha pili, kulibadilisha mambo,” Onyeka alikiri.

“Hata mmoja wa wachezaji kutoka Congo alisema vivyo hivyo. Victor alipoondoka, iliwapa mabeki mapumziko kidogo.”

Pia unaweza kusoma

Mbio za Kombe la Dunia

k

Chanzo cha picha, Getty Images

Ingawa Onyeka amekuwa na jukumu muhimu kwa Nigeria katika miaka michache iliyopita, kiungo huyo amekuwa akipambana kupata namba katika kikosi cha kwanza huko Brentford.

Bado hajaanza mchezo wowote wa Ligi Kuu England msimu huu chini ya meneja mpya Keith Andrews na alitumia msimu uliopita kwa mkopo akiwa Augsburg katika Bundesliga.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 anasema alijitahidi katika maandalizi yake ya kiakili wakati akicheza nchini Ujerumani.

“Ni vizuri kwa sababu ukiwa na msongo wa mawazo, unajaribu tu kuwa mtulivu kadiri iwezekanavyo,” ameeleza.

“Najaribu kufanya hivyo kila siku, lakini mara nyingi hufanya hivyo kabla ya michezo, ili tu kujiandaa.”

“Nafanya hivyo chumbani kwangu kabla ya kwenda uwanjani na baada ya kipindi cha kwanza najaribu kufanya kidogo. Nazingatia tu kupumua kwangu ili kuhakikisha nimetulia.”

Ingawa Onyeka alicheza kwa dakika nyingi akiwa na Augsburg, alishindwa kupata bao katika mechi 34 katika mashindano yote.

Lakini mabao yake yalikuwa muhimu kwa juhudi za Nigeria kufikia Kombe la Dunia mwaka ujao, akifunga bao dakika ya 91 dhidi ya Benin na kuipeleka timu yake kwenye mechi za mchujo, kabla ya pia kufunga bao kabla ya kutolewa na DR Congo.

“Inasikitisha kwamba hatukufuzu Kombe la Dunia lijalo, licha ya vipaji tulivyonavyo. Ni motisha kwetu kwenda Afcon na kushinda na kulirudisha kombe nyumbani.”

‘Kocha mwenye upendo’

k

Chanzo cha picha, EPA

Onyeka anasema pia amejadiliana malengo yake na kocha wa Nigeria, Eric Chelle, raia wa Mali ambaye alichukua nafasi hiyo mwezi Januari na kufufua juhudi za Super Eagles za kufikia Kombe la dunia ambazo hazikufanikiwa.

“Nadhani aliingia na kubadilisha kila kitu – jinsi tunavyocheza, jinsi tulivyopangwa, na falsafa yake ni nzuri sana,” amesema Onyeka.

“Ni kocha mwenye upendo. Jinsi anavyozungumza na wachezaji, anataniana na wachezaji. Yuko tofauti ikilinganishwa na kile tulichokuwa nacho hapo awali.”

Hata hivyo, Chelle yuko katika majonzi ya kuwakosa nahodha, William Troost-Ekong 32, ambaye alitangaza kustaafu mechi za kimataifa licha ya kutajwa katika kikosi cha awali.

Beki mwingine wa kati Benjamin Frederick 20, naye atakosa, kama Onyeka yuko kwenye orodha ya Brentford, na alivutia sana baada ya kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Nigeria chini ya Chelle, lakini atakosa mashindano hayo nchini Morocco baada ya kuumia goti lake akiwa kwa mkopo nchini Ubelgiji.

“Ni pigo kubwa kwetu kwa sababu Benjamin amejiunga na timu (ya Nigeria) na kila mtu anampenda,” alisema Onyeka.

“Kuichezea Nigeria ni kazi kubwa, lakini tumezoea.”

“Ukiona baadhi ya maoni kila tunapopoteza michezo, inakera. Lakini nawaelewa (mashabiki) kwa sababu hili ni jambo wanalolipenda.”

“Mpira wa miguu ni kitu kinachowafanya watu kuwa na furaha, kinachowaleta watu pamoja. Kila wakati Nigeria inapocheza, kila mtu anavutiwa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *