Dhoruba na baridi kali zimesababisha vifo vya Wapalestina 17 katika Ukanda wa Gaza tangu mwanzoni mwa mwezi huu, kwa mujibu wa serikali za mitaa Gaza, huku Israel ikishadidisha vikwazo vikali vya kuingia kwa vifaa vya kuunda makazi na misaada mingine ya kibinadamu katika eneo hilo la Palestina lililokumbwa na vita.

Kwa mujibu wa Idaya ya Ulinzi wa Raia ya Palestina huko Gaza, kwa uchache watu 17 tayari wameshapoteza maisha yao ndani ya mwezi huu wa Disemba, huku mvua kubwa, upepo mkali na baridi kali zikiharibu makazi ya wakimbizi wa ndani na kusababisha kuta, nyumba na mahema, mengi ambayo tayari yameharibiwa na mashambulizi ya Israel, kuanguka.

Vyanzo vya matibabu huko Gaza vimesema miongoni mwa walioaga dunia kwenye majanga hayo ni watoto wanne, ambao walifariki dunia kutokana na baridi shadidi.

Msemaji wa Idara ya Ulinzi wa Raia Gaza, Mahmoud Bassal amesema katika taarifa kwamba, “nyuzijoto hupungua sana wakati wa saa za usiku,” akionya kwamba “baridi kali inahatarisha maisha ya watoto wadogo ambao hawana makazi wala vifaa vya kupasha joto.”

Afisa huyo wa Gaza ameongeza kuwa, “Tunachopitia sasa Gaza ni janga la kibinadamu. Waokoeni watoto wa Gaza kabla ya baridi kuwaua.”

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 140,000 wameathiriwa na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko katika maeneo zaidi ya 200 ya wakimbizi katika Ukanda wa Gaza.

Wakati huo huo, imeelezwa kuwa, mvua kubwa zinazoendelea kunyesha huko Gaza hadi hivi sasa zimeshaharibu asilimia 90 ya mahema ya wakimbizi wa ukanda huo, wakati huu wa msimu wa baridi kali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *