Waziri Mkuu wa Qatar ameonya kwamba, ukiukaji unaofanywa kila siku wa Israel wa makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza unatishia mchakato mzima wa mapatano hayo, huku akitoa wito wa kutekelezwa haraka awamu inayofuata ya makubaliano hayo ili kukomesha vita vya mauaji ya halaiki vya Israeli dhidi ya eneo la Wapalestina lililozingirwa.

Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani ametoa kauli hiyo kufuatia mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio huko Washington jana Jumatano, ambapo amesisitiza kwamba “ucheleweshaji na ukiukwaji wa usitishaji mapigano huhatarisha mchakato mzima na kuwaweka wapatanishi katika hali ngumu”.

Waziri Mkuu wa Qatar, ambaye nchi yake ina jukumu muhimu la upatanishi, alisema misaada ya kibinadamu lazima ifike Gaza “bila masharti” na kwamba awamu ya pili ya makubaliano lazima ianze mara moja.

Mazungumzo hayo kwenye mkutano wa saba wa kimkakati ya Marekani na Qatar yanakuja huku makubaliano hayo dhaifu yakiendelea kuyumba, na hali ya kibinadamu ikizidi kuwa mbaya kote Gaza.

Haya yanajiri katika hali ambayo, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina HAMAS imeushutumu utawala wa Kizayuni wa Israel kwa ukiukaji mkubwa na uliopangwa wa makubaliano hayo ya kusitisha vita, ikionya kwamba kuendelea kwa mwelekeo huo kunayaweka makubaliano hayo katika hatari ya kuvunjika kikamilifu.

Tangu kuanza kutekelezwa makubaliano ya usitishaji mapigano mwezi Oktoba, Israel imeendelea kushambulia maeneo mbalimbali ya Gaza kila siku (zaidi ya mara 800 mpaka sasa), na kuua shahidi watu karibu 400 – katika ukiukaji wa wazi wa makubaliano hayo, kwa mujibu wa mamlaka za Gaza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *