
Rais wa Russia, Vladimir Putin amepuuzilia mbali madai ya Magharibi kuhusu shambulio ‘tarajiwa’ kutoka Moscow na kuyaeleza kuwa “uongo na upuuzi,” akisisitiza kwamba kauli hizo zinatolewa kwa makusudi ili kushadidisha hali ya taharuki na wasiwasi katika eneo.
Akizungumza katika mkutano wa Bodi ya Wizara ya Ulinzi jana Jumatano, Putin alibainisha kuwa hali ya jiopolitiki duniani bado ni “tete” na “hasasi mno” katika baadhi ya maeneo.
Ameshutumu nchi wanachama wa NATO kwa “kujiandaa kwa vita vikubwa” kwa kujenga na kuboresha vikosi vyao vya mashambulizi, huku “zikiwahadaa” wananchi wao kwa madai ya kujongea mapigano yasiyoepukika na Russia.
“Nakariri kusema kwamba huu ni uwongo, upuuzi, upumbavu mtupu kuhusu eti uwepo wa tishio fulani la Russia kwa nchi za Ulaya. Lakini hili linafanywa kwa makusudi kabisa,” Putin amesema, akiongeza kuwa maafisa wa EU “wamesahau jukumu lao” na wanaongozwa na maslahi ya binafsi au ya kisiasa ya muda mfupi.
Amesisitiza kwamba, katika historia yake yote, hata katika hali ngumu zaidi, Russia imekuwa ikijitahidi kila wakati kutafuta suluhu za kidiplomasia kwa migogoro na mizozano, mradi tu kuna fursa japo ndogo. “Jukumu la kutokumbatia fursa hizi liko kwa wale walioamini wanaweza kuzungumza nasi kwa kutumia nguvu na mabavu,” Putin ameongeza.
Rais wa Russia amesema kwamba, Moscow inaunga mkono “ushirikiano wenye usawa na wenye maslahi ya pande zote” na Marekani na mataifa ya Ulaya, pamoja na uundwaji wa mfumo jumuishi wa usalama katika eneo lote la Eurasia.