Kundi la waasi wa M23 limeanza kujiondoa katika mji wa kimkakati wa Uvira,mashariki mwa nchi hiyo. Waasi hao walichukua udhibiti wa mji huo wiki iliyopita kufuatia mashambulizi waliyoyaendesha mapema mwezi huu, licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani. 

Taarifa za kuanza kujiondoa kwa waasi wa M23 katika mji wa Uvira zimethibitishwa na uongozi wa kundi hilo pamoja na mamlaka za eneo hilo.

Usiku wa kuamkia leo, kiongozi wa kisiasa wa M23, Bertrand Bisimwa, aliliambia shirika la habari la AP kwa njia ya simu kwamba zoezi la kujiondoa litakamilika mapema leo.

Ikumbukwe kuwa mwanzoni mwa wiki hii, waasi wa M23 walitangaza nia yao ya kujiondoa kutoka mji huo wa kimkakati kufuatia ombi la Marekani lililotaka waondoke mara moja.

Mji wa Uvira, ulioko karibu na mpaka wa DRC na Burundi, uliangukia mikononi mwa waasi hao Jumatano iliyopita, baada ya M23 kuteka miji mikubwa ya Goma na Bukavu mapema mwaka huu.

 Kongo Rubaya 2025 | M23
Mwanajeshi wa M23 akiwa amesimama katika eneo la machimbo la RubayaPicha: Camille Laffont/AFP

Kuiteka Uvira kuliwapa waasi hao udhibiti wa mpaka wa ardhini kati ya DRC na Burundi, na hivyo kuizuia serikali ya Kongo kupata msaada wa kijeshi kutoka kwa jirani yake huyo.

Mashambulizi ya M23 yalilaaniwa vikali na Marekani, iliyosema hatua hiyo ilikuwa ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya amani yaliyosainiwa kati ya serikali za DRC na Rwanda, chini ya usimamizi wa Washington wiki chache zilizopita.

Baada ya mashambulizi hayo, Marekani iliishutumu Rwanda kwa kuunga mkono hatua za M23, ikionya kuwa utawala wa Rais Donald Trump utachukua hatua dhidi ya yeyote atakayekiuka makubaliano hayo.

Lakini wakazi wa Uvira wamepokeaje taarifa za kujiondoa kwa waasi hao?DW imezungumza na baadhi yao, na haya ni maoni yao.

Trump I Kagame I Tshisekedi
Rais wa Marekani Donald Trump akiwa pamoja na rais wa Rwanda Paul Kagame na mwenzake wa DRC Felix Tshisekedi Picha: Andrew Caballero-Reynolds/AFP

Mkaazi wa kwanza ”Kuondoka kwao kunatusaidia sana, tunahitaji kuwa na amani, amani ndio lengo namba moja na hatutaki jinsi mambo yalivyokuwa kwamba hatuwezi kusafiri kwenda Bukavu wala wa Bukavu hawawezi kuja Uvira”

Mkaazi wa pili Tunahitaji amani, sisi raia tunahitaji amani, hao kuondoka ni vizuri na serikali itajua jinsi ya kufanya huko mbeleni”

Swali linalosalia ni mustakabali wa usalama wa mji wa Uvira baada ya kuondoka kwa M23. Haya ni maoni ya mmoja wa wakazi wa mji huo.

Mkaazi wa tatu ” Usalama wetu tunauhofia kabisa kwa sababu hili eneo lilikuwa na vita, makundi yalikuwa yakipigana na wakati ambapo M23 wanaondoka hatujui nani anayekuja “

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni miongoni mwa migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu duniani, huku zaidi ya watu milioni saba wakilazimika kuyahama makazi yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *