Mfungaji Bora wa muda wote wa Nigeria katika Kombe la Dunia, Ahmed Musa jana Jumatano, Desemba 17, 2025 amestaafu rasmi kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo ‘Super Eagles’.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 33, ametangaza uamuzi huo wa kutoendelea kuitumikia timu ya taifa ya nchi hiyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.
“Nimevaa beji hii kwa ufahari kwa miaka 15. Tangu nikiwa mvulana wa miaka 17 aliyepokea kila wito wa Nigeria hadi kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi wa Super Eagles kwa mechi 111.
“Bingwa wa AFCON 2013. Mfungaji mwenye mabao zaidi wa Nigeria katika Kombe la Dunia. Mtumishi wa unahodha, muumini, nimetoa kila kitu.
“Asante Nigeria. Moyo wangu daima utabakia kuwa kijani,” amesema Musa.
Aliyewahi kuwa mchezaji wa timu ya Taifa ya Nigeia, Ahmed Mussa. Picha na Mtandao.
Mwaka 2014 katika Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Brazil, Ahmed Musa aliweka rekodi ya kuwa Mfungaji Bora wa Nigeria katika Kombe la Dunia baada ya kufunga mabao mawili katika mchezo dhidi ya Argentina.
Pia anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji pekee wa Nigeria kufunga katika Fainali mbili tofauti za Kombe la Dunia.
Musa alianza kuitumikia timu ya Taifa ya Nigeria kwa mara ya kwanza Septemba 5, 2010 katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za AFCON 2012, wakati huo alikuwa na umri wa miaka 17 tu.
Amekuwa nahodha wa timu ya taifa ya Nigeria tangu 2019 baada ya John Obi Mikel kustaafu kuichezea timu hiyo.
Uamuzi wa Musa kustaafu kuichezea Nigeria umekuja wiki mbili baada ya nyota mwingine wa nchi hiyo, beki William Troost-Ekong kutangaza kutoendelea kuitumikia tena timu ya taifa ya nchi hiyo.