
Refa mstaafu wa kimataifa wa Tanzania, Victor Mwandike, amefariki dunia leo Alhamisi Desemba 18, 2025 jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT), imesema Mwandike amefariki akiwa anapatiwa matibabu.
“Mwenyekiti Ndugu Emmanuel Chaula kwa masikitiko makubwa amepokea taarifa ya kifo cha mwamuzi mstaafu wa kimataifa wa FIFA, Victor Mwandike, kilichotokea leo tarehe 18 Desemba 2025 katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
“Marehemu Victor Mwandike alikuwa mmoja wa waamuzi waandamizi waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya waamuzi nchini na kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu.
“Hadi umauti unamkuta marehemu alikuwa mkufunzi wa waamuzi na mjumbe wa kamati ya waamuzi ya TFF kwa nyakati tofauti tofauti.
“FRAT inatoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na jamii ya soka kwa ujumla katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo,” imefafanua taarifa ya FRAT.
Mwandike anakumbukwa kwa historia yake ya kutoa kadi tatu nyekundu katika mechi moja ya Watani wa Jadi ‘Kariakoo Derby’ baina ya Simba na Yanga, Oktoba 26, 2008.
Katika mechi hiyo ambayo Simba ilifungwa bao 1-0, Mwandike alitoa kadi nyekundu kwa Haruna Moshi ‘Boban’ na Meshack Abel wa Simba pamoja na Bernard Mwalala wa Yanga ambaye ndiye aliyefunga bao hilo pekee.
Boban alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kuonekana akimpiga kibao beki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akidai alimchezea rafu ya kumrukia, huku Abel na Mwalala kadi zao nyekundu zilitokana na kutishiana kupigana.