Augustin Minani, amebainisha kuwa kati ya wakimbizi elfu tano hadi elfu kumi tayari wameingia kuomba hifadhi, huku kukiwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa misaada ya kibinadamu.

Tarafa ya Rumonge, iliyoko kusini mwa Burundi na inayopakana kwa kiasi kikubwa na Ziwa Tanganyika, imekuwa kituo kikuu cha kuwapokea wakimbizi wanaokimbia mapigano yanayoendelea katika maeneo ya Fizi na Baraka kusini mwa jimbo la Kivu Kusini, Mashariki nchini DRC.

Baadhi ya wakimbizi hao wanasema wanakimbia mapigano makali yanayoendelea katika maeneo ya Makobora, njiani kutoka Uvira kuelekea miji ya Fizi na Baraka. Wanasema hutumia mitumbwi na boti ndogo kuvuka Ziwa Tanganyika ili kufika Rumonge, Burundi. Wakimbizi hao wanalalamikia hali ngumu wanazokutana nazo mara tu baada ya kuwasili Rumonge. Wanasema hakuna chakula, hawana sehemu ya kulala, hakuna vyoo wala maji safi ya kunywa.

Kongo na Rwanda: Nini kipo kwenye mkataba wa amani?

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Kwa mujibu wa Mkuu wa Tarafa ya Rumonge, Augustin Minani, tarafa hiyo imeelemewa kabisa. Anasema kila siku mitumbwi na boti huwasili zikiwa zimejaa wakimbizi. Maeneo yote yaliyotengwa kwa mapokezi yamefurika.

Minani anasema wakimbizi wamesambaa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo bandarini wanapowasili, uwanja wa mpira na kituo cha muda kilichotengwa kuwapokea, ambacho nacho kimejaa.

“Tayari tumezidiwa. Kituo cha muda kilichotayarishwa kuwapokea kimejaa. Hata uwanja wa mpira umefurika, na nje ya uwanja wakimbizi ni wengi sana. Isitoshe, hata bandarini wanakowasili kumefurika. Hatuna mahali pa kuwaweka.”

UNHCR: Imewasajili wakimbizi zaidi ya 40,000 kuanzia Desemba 

Mkuu huyo wa tarafa ametoa wito kwa wahisani na watu wote wenye moyo wa kujitolea kutoa misaada ya haraka kwa wakimbizi hao. Ripoti zinaeleza kuwa mkimbizi mmoja amefariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, wakimbizi hao wanatakiwa kuondolewa Rumonge na kuhamishiwa Busuma, katika tarafa ya Rutana, ambako kambi mpya inatarajiwa kuanzishwa.

UNHCR |
Shirika la kuwahudumia wakimbizi UNHCRPicha: Michael Varaklas/AP Photo/dpa/picture alliance

Kwa upande wake, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) linasema kuwa tangu tarehe 5 Desemba, tayari limewasajili zaidi ya wakimbizi 40,000 waliovuka mpaka kuingia Burundi kuomba hifadhi.

Wimbi hili la wakimbizi linaendelea kuingia Burundi licha ya mpaka wa nchi hiyo kufungwa, baada ya waasi wa M23 kuuteka mji wa Uvira wiki iliyopita.

Hali hii inajiri wakati wakimbizi wa Burundi waliokuwa katika kambi za Kigoma, Tanzania, wakiendelea kurejeshwa nchini mwao. Hivi karibuni, zaidi ya wakimbizi elfu moja waliwasili Burundi, baadhi yao wakidai kuwa walirejeshwa bila hiari yao.

Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano wa pande tatu kati ya Tanzania, Burundi na UNHCR uliofanyika Tanzania. Serikali ya Tanzania ilitangaza kuwa ifikapo Juni 2026, wakimbizi wote wa Burundi wanapaswa kuwa wamerejea nchini kwao.

Serikali ya Burundi imekuwa ikiwahakikishia wakimbizi wanaorejea kuwa hali ya usalama nchini iko shwari, na kwamba wanapowasili hupewa msaada wa kifedha unaowawezesha kugharamia mahitaji yao ya msingi kwa kipindi cha miezi mitatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *