Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.Ashatu Kijaji amewahamasisha watanzania kutumia mapumziko ya mwisho wa mwaka kwa kufanya utalii katika hifadhi ya Taifa Kitulo, Mpanga Kipengere na kwenye vivutio vingine vya utalii nchini ili kufaidi urithi wa kipekee wenye vivutio adimu Duniani.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo alipoitembelea hifadhi hizo Mkoani Njombe, kwa lengo la kukagua shughuli za uhifadhi ikiwa ni hatua muhimu ya kuongeza chachu katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyomo kusini mwa Tanzania kimataifa.
Waziri Kijaji amesema kuwa Wizara, imejipanga kikamilifu kuwahudumia vyema watalii wote kwa viwango vya kimataifa na kumfanya mtalii kurudi zaidi ya maramoja kufaidi urithi wa hifadhi nchini.
Aidha, Waziri Kijaji ameilekeza Shirika la Uhifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuendelea kuibua mazao mapya ya utalii, ili kuendana na kasi ya wingi wa watalii wanaoingia nchini ambayo ni matokeo chanya ya Serikali.
Amezitaka TANAPA na TAWA kufungua zaidi milango kwa wawekezaji katika kuboresha miundombinu ndani ya hifadhi hiyo ikiwemo maeneo ya michezo, malazi na barabara huku akisisitiza kutumia vijana kunadi uzuri na upekee wa Hifadhi ya Kitulo katika kuvutia watalii.
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Hamad Hassan Chande, amewapongeza wananchi kwa kazi nzuri ya uhifadhi na kuwahamasisha kuendelea kushirikiana na Wizara hiyo katika kuhifadhi endelevu rasilimali zilizopo kwa maslahi mapana ya Taifa na mtu moja moja.
Katika ziara hiyo, pia Dkt. Kijaji ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Nkoba Mabula, pamoja na viongozi wengine wa Wizara hiyo.
#StarTvUpdate