
Siku tatu kabla ya kuanza kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 huko Morocco, Zambia imepata pigo baada ya Kocha wake Mkuu, Moses Sichone kuzuiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kusimamia timu kwenye mashindano hayo.
Sababu iliyofanya Sichone azuiwe ni kutokuwa na leseni inayokidhi vigezo vya kulisimamia benchi la ufundi kwenye AFCON.
Sichone ana leseni Daraja A ya Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA) na ili akidhi vigezo vya kusimamia timu anatakiwa awe ama na ile ya juu zaidi Ulaya ‘Pro Licence’ au leseni Daraja A ya CAF.
Sichone alianza kuinoa Zambia mwezi uliopita akirithi mikoba iliyoachwa wazi na Avram Grant ambaye alitimuliwa na Chama cha Soka Zambia (FAZ) baada ya mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Dunia.
FAZ sasa inapambana na muda kusaka Kocha Mkuu mpya kabla ya mchezo wao wa kwanza kwenye Fainali hizo ambao watacheza na Mali, Desemba 22, 2025.
Fainali za AFCON 2025 zitaanza Jumapili, Desemba 21, 2025 kwa mchezo baina ya Comoro na wenyeji Morocvo katika Uwanja wa Prince Moulay Hassan, Rabat.
Morocco, Mali, Zambia na Comoro ndizo timu zinazounda kundi A la mashindano hayo.