Tabia ya kutovaa viatu kwa wenye kisukari ni hatari kwasababu naweza kusababisha madhara ma-kubwa kwenye miguu, ambayo mara nyingine inaweza kuleta matatizo sugu ikiwa hayatachukuliwa tahadhari mapema na kuleta ulemavu wa miguu.

Watu wenye kisukari wapo katika hatari kubwa ya kupata vidonda vya miguu kwa sababu kama mgonjwa atashindwa kabisa kudhibiti viwango vya sukari kwa muda mrefu inaweza kuharibu mishipa ya neva pamoja na kuharibu mishipa ya damu na kusababisha mzunguko wa damu kuwa dhaifu na hivyo kuanza kutengeneza hali ya ganzi kwenye nyayo za miguu kwa ujumla.

Hii inamaanisha kuwa miguu inaweza kushindwa kuhisi maumivu ya kujichoma na kitu chenye ncha kali au kuungua kwa moto kwa sababu ya ganzi.

 Kwa hivyo, kama mgonjwa ikiwa amefikia hali ya miguu kuwa na ganzi na kupoteza hisia, ni muhimu kuacha kutembea bila kuvaa viatu kwa sababu hata kiasi kidogo cha maji ya moto mguuni kinaweza kumletea lengelenge na kutengeneza kidonda pasipo kuhisi maumivu na atajua kama kuna kidonda mguuni mpaka pale kidonda kitavyoanza kutoa harufu.

Kutembea bila viatu pia huongeza hatari ya kupata maambukizi ya ngozi. Vijidudu na bakteria vinavyo-patikana ardhini vinaweza kuingia kwenye ngozi iliyo na kidonda kidogo kisichoonekana.

Wenye kisukari wanapata ugumu zaidi kupona kutokana na mfumo wa kinga mwilini ambao unakuwa dhaifu kutokana na kiwango cha juu cha sukari. Hii inaweza kusababisha maambukizi makali na vidonda visivyopona.

Viatu hutoa kinga ya moja kwa moja kwa miguu. Viatu vinapunguza uwezekano wa kukatwa miguu au sehemu ya mguu, kupasuka kwa ngozi au kupata vidonda.

 Aidha, soksi safi, kavu na zisizobana husaidia kuondoa unyevu na kuzuia ngozi kugusana moja kwa mo-ja na viatu, jambo linalopunguza vidonda zaidi.

Baada ya kumaliza kuoga au kunawa miguu, lazima kukausha miguu vizuri hasa katikati ya vidole ili kuepusha malengelenge.

Wataalamu wanashauri watu wenye kisukari kuvaa viatu kila wakati hata ndani ya nyumba, hasa ikiwa kuna sakafu ngumu. Tumia kioo kukagua miguu kila siku ili kuona kama kuna vidonda.

Kwa ujumla, kutembea bila viatu ni hatari kwa mtu mwenye kisukari kwani miguu inaweza kuumia bila kujua, kuambukizwa na kusababisha matatizo makubwa.

Miguu ni msingi wa mwili, hivyo kuilinda ni sehemu muhimu ya kudhibiti kisukari na kuishi maisha yenye afya

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *