Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la idadi ya watu wanaopata kiharusi duniani, Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi zilizoathirika.

Wataalamu wa afya wanasema kiharusi ni ugonjwa wa ghafla unaotokana na ubongo kukosa hewa na virutubishi kutokana na kuziba au kupasuka kwa mishipa ya damu inayosambaza damu kwenye ubongo.

 Shinikizo la juu la damu linaweza kusababisha kupasuka kwa mishipa hiyo, huku mafuta mengi ya-kiganda na kuziba mishipa mingine.

Wagonjwa wanaweza kupooza, kushindwa kuongea, kupoteza kumbukumbu, au hata kifo.

Kwa watu waliowahi kupata kiharusi, hatari ya kupata tena ni kubwa, na hatari ya kifo inategemea aina ya kiharusi.

Kiharusi kinachosababishwa na kuvuruga mishipa ya damu ni hatari zaidi kuliko kiharusi cha kuziba mishipa.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa kila mwaka, watu milioni 15 hupata kiharusi.

Kati yao, milioni tano hufa, na wengine milioni tano hubaki na ulemavu wa kudumu, jambo linalosaba-bisha mzigo mkubwa kwa familia na jamii.

Nchini Tanzania, wagonjwa wa kiharusi wanaongezeka. Wataalamu wa afya wanatoa tahadhari kuwa hali hii inaweza kuathiri vijana na wazee endapo hatua za mapema hazitachukuliwa.

 Taasisi za afya kama Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando zinashuhudia ongezeko hili.

 MOI inaripoti kupokea wagonjwa watatu hadi sita kwa wiki waliopata kiharusi cha kupasuka kwa mshipa wa damu, wakati BMH inapokea wagonjwa wawili hadi watatu kwa siku.

Sababu za kiharusi

Dk Sunday Mazigo, mtaalamu wa magonjwa ya binadamu na mtafiti anasema sababu zinazosababisha kiharusi ni pamoja na shinikizo la juu la damu, uvutaji wa sigara, unywaji pombe kupita kiasi, ugonjwa wa moyo, ulaji usiofaa (ikihusisha mafuta mengi, chumvi, na sukari), msukumo wa juu wa damu, kisu-kari, na ukosefu wa mazoezi.

 “Sababu kuu ya kiharusi ni kuziba kwa mishipa ya damu hasa ile iliyopo kwenye ubongo. Damu ikiwa haipiti vizuri kwenye mishipa hiyo, baadhi ya sehemu za mwili hazitafanya kazi ipasavyo. Shinikizo la damu linachangia kwa kiasi kikubwa, pamoja na urithi kutoka kwa wazazi,” anasema.

WHO inasisitiza kuwa kwa kila wagonjwa 10 wanaokufa kutokana na kiharusi, wengi wangeokolewa kama shinikizo la damu lingedhibitiwa mapema. Kwa watu wenye umri wa chini ya miaka 65, takriban wawili kati ya watano vifo vyao vinahusiana na uvutaji sigara.

 Kiharusi kwa vijana

 Dk Joshua Willey, mtaalamu wa neva na daktari bngwa wa kiharusi katika Chuo Kikuu cha Colombia, Marekani, anasema ingawa wengi huona kiharusi kama ugonjwa wa wazee, viwango vya kiharusi kwa vijana vinaongezeka.

 Ripoti ya Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vya Marekani (CDC) inayoangalia vipindi vya mwaka 2011/13 na 2020/22 inaonyesha ongezeko la asilimia nane kwa maambukizi ya jumla ya kiharusi, huku ongezeko kubwa zaidi likiwa kwa watu wa umri wa miaka 18 hadi 44 (asilimia 14.6) na miaka 45 hadi 64 (asilimia 15.7).

“Kuongezeka kwa unene uliopitiliza na hali nyingine za kiafya kama kisukari miongoni mwa vijana, kunasababisha magonjwa ya moyo kuanza mapema na kuongeza hatari ya kiharusi katika umri mdogo,” anasema.

Ripoti ya Tume ya Shirika la Kiharusi Duniani (WSO) inatabiri ongezeko la asilimia 50 la wagonjwa wa kiharusi kufikia mwaka 2050, litakalosababisha vifo vya watu milioni 9.7 kila mwaka. Zaidi ya asilimia 90 ya vifo hivyo vitatokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati. Ulemavu unaohusiana na kiharusi pia unaongezeka kwa kasi katika nchi hizi.

 Profesa Sheila Martins, Rais wa WSO, anasema: “Maangamizi yanayosababishwa na vifo na ulemavu kutokana na kiharusi si jambo lisiloepukika. Kiharusi kinaweza kuzuilika kwa kiwango kikubwa kwa kudhibiti sababu za hatari zinazojulikana kama shinikizo la damu, uvutaji sigara, ukosefu wa mazoezi, kisukari, kolesteroli ya juu, tumbaku na pombe. Hatari hizi zinachangia takriban asilimia 90 ya matukio yote ya kiharusi.”

 Dalili za kiharusi

Dalili hujitokeza ghafla na hutofautiana kulingana na sehemu ya ubongo iliyoathirika. Miongoni mwa dalili hizo udhaifu au kupoteza ganzi upande mmoja wa mwili au uso, ugumu wa kuzungumza, kushindwa kumeza, kutofahamu kinachoendelea, kuchanganyikiwa, kushindwa kudhibiti misuli, shida ya kuona, na maumivu makali ya kichwa bila sababu.

 Dk Mazigo anashauri: “Njia za kupunguza uwezekano wa kiharusi ni kuepuka uvutaji wa sigara, kupun-guza pombe, kula vyakula vyenye afya, epuka mafuta mengi, sukari na chumvi, fanya mazoezi ya mwili angalau dakika 30 kila siku, dhibiti uzito na shinikizo la damu, na chunguza afya yako mara kwa mara.”

 Kiharusi kwa watoto wenye seli mundu

 Utafiti uliofanywa na Dk Emmanuela Ambrose, Daktari Bingwa na Mkuu wa Kitengo cha Selimundu Hospitali ya Bugando, unaonesha kuwa kati ya watoto 196 wenye seli mundu, 47 walikuwa hatarini ku-pata kiharusi. Watoto waliopatikana hatarini walianzishiwa dawa ya ‘Hydroxyurea’, na utumiaji wa ul-tras sound ya Dopla ya kichwa ulionyesha kuwa kasi kubwa ya mtiririko wa damu kwenye mishipa mikuu ya ubongo inahusiana na hatari ya kiharusi.

Baada ya miezi 12 ya matibabu, asilimia 83 ya watoto waliopokea dawa walifikia utengamafu bila kiha-rusi au vifo vinavyohusiana na dawa. Watoto wenye bandama kubwa walihitaji dozi ndogo, ambayo iliboresha kiwango cha damu na fetal haemoglobin (HbF).

 Ushuhuda wa wagonjwa

Joseph Atanas aliyewahi kupata kiharusi cha muda, anasema: “Nilianza kupoteza nguvu upande mmoja wa mwili, hivyo nikakimbia kwenda Hospitali ya Bugando. Madaktari walifanya vipimo vya shinikizo la damu, sukari, na mtiririko wa damu kwenye ubongo. Nikaambiwa nina kiharusi cha muda mfupi, ni-kaanza matibabu ya kuzuia damu kuganda na kudhibiti shinikizo la damu. Matibabu hayo yalisaidia ku-punguza hatari ya kuwa na kiharusi kikubwa. Baada ya kutumia dawa hali yangu iliendelea vizuri; sija-wahi kupata hali hiyo tena. Nazingatia maelekezo ya daktari, kufanya mazoezi, kula vizuri na niliacha kabisa kutumia kilevi.” 

Naye mkazi wa Buhembe mkoani Kagera, Adil Mutalemwa anasema alianza kuumwa sana kichwa, macho na moyo kwenda kwa kasi.

Alipokwenda hospitalini iligundulika ana shinikizo kubwa la  damu  na kuanza kutumia dawa kwa mwa-ka mmoja kisha akaacha.

“Baada ya kuona nimepata nafuu na presha kurudi kawaida niliacha dawa, miezi sita kupita tangu nil-ivyoacha dawa hali yangu ilibadilika. Nilikuwa  siwezi kuinua mguu mmoja, mkono na mdomo pia ulian-za kwenda upande. Ikabidi nirudishwe tena hospitali ambapo nilianzishiwa dawa upya na mazoezi ti-ba,” anasema.

Anasema kwa sasa hali yake inaendelea vizuri, akieleza kuwa dawa na mazoezi vilimsaidia na hali inar-udi taratibu japokuwa kwa sasa anatembea kwa usaidizi huku  akiendelea kutumia dawa za presha ya juu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *