BAADA ya Tanzania Bara wakati huo ikiitwa Tanganyika kupata uhuru katika miaka ya 1961, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alianzisha vita dhidi ya maadui watatu; ujinga, maradhi na umaskini. Nyerere akahimiza Watanzania kushiriki vita hiyo kikamilifu. Kimsingi, Nyerere alikuwa katika njia sahihi.
Kwamba, Tanganyika (Tanzania Bara) na hata Tanzania kwa ujumla ikifanikiwa kupigana na maadui hao watatu, itageuka kuwa ‘kisiwa cha amani na ‘kisiwa cha maendeleo’ na maisha ya hadhi ya juu. Makala haya yanaonesha namna maadui hao wanavyojitahidi kuungana na kuwashambulia Watanzania kwa kile inachosema wamejipa jina la umoja la ‘ugonjwa.’
Wakati Watanzania wanaendelea kutafakari maadhimisho ya Miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika, hawana budi kukumbuka alichosema Nyerere kuwa, “Msingi wa maendeleo ya watu wetu ni kupambana na umaskini; bila kufanya hivyo, uhuru wetu hauna maana.”
Aliongeza: “Tusipojenga uchumi wetu tukabaki kuwa masikini, tutakuwa tumeshindwa na tutaendelea kuwa tegemezi.” Mintarafu ujinga, vyanzo mbalimbali vya kisiasa na kihistoria vinamnukuu Mwalimu Nyerere akisema,”Ujinga ni adui mkubwa wa maendeleo. Lazima tupambane nao kwa nguvu zote kupitia elimu.”
Anaongeza: “Nchi masikini haiwezi kujenga maendeleo ya maana bila kwanza kumkomboa mtu wake kutoka kwenye ujinga.” Akizungumzia adui wa tatu, muasisi huyo wa taifa anasema maradhi (magonjwa) ni moja ya vikwazo vikubwa vya maendeleo kwa kuwa hakuna taifa litakaloendelea wakati watu wake wanauguaugua.
Hii ina maana kuwa, watu wagonjwa (kwa muktadha huu; wa kimwili na kiroho) hawawezi kushiriki ipasavyo vita dhidi ya umaskini wala ujinga na badala yake, watakuwa legelege. Kibaya zaidi, ni pale watakapougua ugonjwa au maradhi ya kushindwa ‘kuona’ baya au zuri kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Hapo, ndipo ‘watu wanaoumwa’ uwezo duni wa kutafakari na ‘kuona mbali,’ watajisalimisha hata kwa watu wa mataifa ya ng’ambo ili wawape fedha za kuganga njaa hata kwa kugeuka na kuuana ndani ya familia na nchi yao.
Kwamba, kwa ugonjwa wa umaskini, ‘mgonjwa’ yupo tayari kumuua baba, mama, ndugu, mtoto au rafiki yake eti kwa kuwa tu, anaunga mkono itikadi za kisiasa za kikundi au chama kingine tofauti na yeye; kisha ategemee kupata nyongeza ya fedha au zawadi ‘zinazonuka damu.’
Mgonjwa wa namna hiyo, yuko tayari kudhuru na hata kuangamiza familia yake, ndugu zake, jirani zake na hata taifa lake eti kwa kuwa hao, wana wana imani tofauti na yake. Katika mazingira ya giza la namna hiyo, ni vigumu kujua na kuamini hao imani yao ni kwa Mungu yupi; ni Mungu huyu wa kweli; Muumba Mbinu na Nchi!
Kimsingi, maradhi ni adui mbaya zaidi kuliko hao wawili yaani umaskini na ujinga maana kwa mtazamo wangu, wote hao ‘wanabebwa na kubwa lao,’ maradhi na kubwa zaidi, afadhali yawe maradhi ya kimwili na kuliko kuwa maradhi ya kiroho au kiakili.
Ndio maana makala yanasema; “Jamii yetu inaumwa.” Maradhi ya kiroho na kiakili hubeba maadui wengine na kuwakumbatia. Hukumbatia umaskini maana hayatoi nafasi ya uzalishaji mali kwa juhudi na maarifa; badala yake, hufungua milango na kutoa muda wote kwa migogoro, vurugu na mapambano yasiyo na mshindi wala mshindwa.
Jamii inaposhambuliwa na adui aitwaye magonjwa; tena magonjwa ya kiroho, haitoi mwanya kwa watoto kuhudhuria masomo, mafunzo na hata kujifunza na kutumia vyema teknolojia kwa ustawi wa jamii, bali muda na nguvu zote huishia ‘kutafuta mchawi’ na kuendeshwa kwa ‘rimoti kontroo’.
Kwa kutawaliwa na ugonjwa wa kiakili au kiroho, mtu atakuwa Ulaya kwa mfano, atasema, “Tuchome nyumba yetu”, kweli tutaichoma nasi au ndugu zetu kuumia, kufariki dunia na mali zetu kuangamia. Wakati huo, yeye na watu wake huko walipo na mali zao, wataendelea kubaki salama huku wakiendela kupaza sauti mtandaoni, “Tuchome tena; tuchome! Eeee! Tuchome!”
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne aliwahi kusema: “Akili za kuambiwa, changanya na zako.” Ndiyo maana Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa anawatahadharisha Watanzania dhidi ya hatari ya kutumbukia katika shimo na janga la migogoro ya kidini.
Anasema hilo ni janga kwani hakuna vita inayovuruga na kuangamiza jamii kama ilivyo vita na chuki za kidini kwa kuwa chuki za kidini huingia ndani ya mioyo ya watu. Chuki za kidini haziishi na hata pale zinapodhaniwa zimekwisha, huwa hazina mshindi wala mshindwa; pande zote haungamia na kupoteza; ni hasara tupu pande zote.
Anabainisha hayo mwanzoni mwa wiki katika Ibada Maalumu ya Kuwekwa Wakfu kwa Askofu Mteule wa KKKT, Dayosisi ya Morogoro, Dk George Pindua. Ibada hiyo imefanyika katika Usharika wa Kanisa Kuu Bungo, mjini Morogoro na kuhudhuriwa na waumini wa dini na madhehebu mbalimbali.
Askofu Malasusa anasema, “Nataka Watanzania walijue jambo moja muhimu; vita (chuki) vya dini na vya kiimani ni vibaya sana. Vinakwenda ndani zaidi kuliko vita vingine vyote.” Anaongeza: “Popote vilipoanzishwa, havijawahi kuisha, wala hakujawahi kutangazwa mshindi.”
Anawahimiza viongozi wa dini nchini hususan maaskofu wa kanisa hilo kuwa chombo cha kuunganisha watu watu badala ya kuwatenganisha kwa misingi ya vyama vya siasa, itikadi, dini au rangi. Katika hafla ya kuapishwa kuongoza Tanzania kwa kipindi cha pili baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 iliyofanyika Dodoma Novemba 3, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan anasema, “Nitumie fursa hii kuwashukuru kwa dhati ya moyo wangu viongozi wa dini waliohimiza amani na upendo katika kipindi chote cha uchaguzi.”
Anasema chuki za kidini huacha alama ya kudumu moyoni kuliko propaganda za kisiasa. “Wanasiasa wakimharibu mtu, wanamharibu kichwani, kichwa kinakubali. Akija mwanasiasa mwingine akasema lililo jema, kichwa kinafuta lile baya na kukubali hilo zuri.” SOMA: Tanzania yapewa 5 kinara kurejesha Amani DRC, ICGLR
Anaongeza: “Lakini ukimharibu mtu kwenye dini, chuki inaingia moyoni na ikishaingia ni hatari zaidi.” Samia anawataka viongozi wa dini kudumu katika mstari wao wa kiroho na kuonesha sura halisi ya majoho yao na kutotumia kivuli cha dini kwa maslahi binafsi. Alisema hakuna kitabu chochote cha dini kinachofundisha kuvuruga nchi, bali mabaya yanayotokea hutokana na nafsi za watu na utashi binafsi.
Baada ya kuwekwa wakfu, Askofu Pindua naye anasema, “Watanzania tumekuwa mfano wa kuishi pamoja licha ya kuwa na dini, makabila na tamaduni mbalimbali.” Anaongeza: “Ni wajibu wetu kulinda misingi hii na kupambana pamoja na chochote kinachotishia amani na utulivu wa taifa letu.”
Katika tukio hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Denis Londo anawataka Watanzania kuendelea kujenga, kulinda na kudumisha amani kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo ya taifa na ustawi wa watu Watanzania wajiandae kusherehekea sikukuu zote za mwisho wa mwaka na nyingine zote za kidini huku wakitafakari na kujiuliza kwa nafasi zao huku wakimtazama Mungu, wanachangiaje kujenga, kuimarisha na kudumisha amani, au licha ya imami zao ndio wasaliti wa amani itokayo kwa Mungu.
Ndio maana makala yanawaweka maadui wote watatu katika kapu moja la ugonjwa. Kufungulia ‘mbwa’ wa machafuko na chuki za kidini ni kusaliti dini na imani zetu na kujiangamiza wenyewe kwani nchini Tanzania hakuna familia au jamii ambayo haina mchanganyiko wa watu wa dini na imani tofauti. Kwa mujibu wa uchunguzi wa HabariLEO, zipo familia ambazo watu wake ni waumini wa dini na madhehebu mbalimbali wakiwamo Waislamu, Wakristo na wa imani nyingine.
