WIZARA ya Fedha imewataka wataalamu wa Ununuzi na Ugavi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ili kuimarisha utawala bora.
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar ametoa wito huo katika hotuba yake iliyosomwa na kwa niaba ya yake na Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Munde, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 16 wa Mwaka wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) unaofanyika jijini Arusha.
SOMA: Trilioni 455/- zahitajika malengo Dira 2050
Balozi Omar amesema ili kufikia malengo ya Dira 2050, ni muhimu kwa PSPTB kutekeleza shughuli zake kwa kuzingatia dira hiyo.

“Serikali imeelekeza kuwa shughuli zote za ununuzi na ugavi nchini ziunganishwe na mfumo wa NeST ili kuleta uwazi, uwajibikaji na kuhakikisha thamani ya fedha,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PSPTB, Jacob Kibona, ametaja baadhi ya mafanikio ya PSPTB kuwa ni pamoja na kusimamia na kuendeleza mitaala ya kitaaluma kwa lengo la kuzalisha wataalamu wenye uwezo.

Ametaja mengine kuwa ni kutoa mafunzo endelevu ya maendeleo ya kitaaluma, pamoja na kuboresha matumizi ya mifumo ya kidijitali ambapo kwa mujibu wake, PSPTB imefanikiwa kuwajengea uwezo wataalamu 3,164 wa ununuzi na ugavi.