Kuku

Chanzo cha picha, Tribune News Service via Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 6

Kwa miaka mingi, wanasayansi wamekuwa wakionya kuwa ugonjwa wa mafua ya ndege, unaojulikana kama H5N1, huenda siku moja ukaweza kuambukiza binadamu kutoka kwa ndege kwa njia hatari, jambo linaloweza kusababisha janga la afya duniani.

Mafua ya ndege (avian influenza) ni aina ya mafua ambayo yamekithiri (ni ya kudumu) katika Asia ya Kusini na Asia ya Kusini-Mashariki, na yamekuwa yakiambukiza binadamu mara chache tangu yalipoibuka nchini China mwishoni mwa miaka ya 1990. Kuanzia 2003 hadi Agosti 2025, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliripoti kesi 990 za H5N1 kwa binadamu katika nchi 25, zikiwemo vifo 475, kiwango cha vifo cha asilimia 48.

Nchini Marekani pekee, virusi hivyo vimeambukiza zaidi ya ndege milioni 180, mifugo ya ng’ombe wa maziwa zaidi ya 1,000 katika majimbo 18, na watu wasiopungua 70, wengi wao wakiwa wafanyakazi wa mashamba, hali iliyosababisha kulazwa hospitalini kwa watu kadhaa na kifo kimoja.

Mnamo Januari, chui milia watatu na chui mmoja mwenye madoa (spotted tiger) walifariki katika kituo cha uokoaji wa wanyamapori katika mji wa Nagpur, India, kutokana na virusi hivyo ambavyo kwa kawaida huambukiza ndege.

Kwa binadamu, dalili za maambukizi ni sawa na zile za mafua makali, ikiwa ni pamoja na homa kali, kikohozi, koo linalouma, maumivu ya misuli, na wakati mwingine kiwambo cha jicho, huku baadhi ya watu wakiwa hawana dalili.

Hatari kwa wanadamu inabaki kuwa ndogo, lakini mamlaka zinafuatilia kwa karibu virusi vya H5N1 kwa mabadiliko yoyote ambayo yanaweza kuifanya iweze kuambukizwa zaidi kati ya wanadamu.

Wasiwasi huu uliwachochea watafiti wa India Philip Sherrian na Gautam Menon wa Chuo Kikuu cha Ashoka kutengeneza mfumo mpya uliopitiwa kisayansi unaoiga jinsi virusi vya H5N1 vinavyoenea kwa wanadamu, na hatua za mapema zinazoweza kuvizuia kabla havijaenea.

Kwa maneno mengine, mfano (modeli) huo, uliochapishwa katika jarida la BMC Public Health, unatumia takwimu halisi na kompyuta kuonesha jinsi mlipuko huo ulivyotokea kwa uhalisia.

“Janga la binadamu linalosababishwa na virusi vya H5N1 ni hatari ya kweli, lakini tunaweza kutumaini kuliepuka kwa kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na kuchukua hatua kwa afya ya umma iwe ya haraka na yenye kubadilika zaidi,” Profesa Menon aliiambia BBC.

Watafiti wanasema janga la mafua ya ndege litaanza kimya kimya, pale ndege mmoja aliyeambukizwa atakapomwambukiza binadamu mmoja, mara nyingi akiwa mkulima, mfanyakazi wa soko au mhudumu wa kuku.

Kuanzia hapo, hatari kubwa si maambukizi ya awali, bali kile kinachoweza kutokea baadaye, yaani kuendelea kwa maambukizi kutoka binadamu kwenda kwa binadamu mwingine.

Kwa kuwa milipuko halisi huanza na data chache na isiyokamilika, watafiti waligeukia jukwaa huria la Bharat Sim, ambalo hapo awali lilitengenezwa ili kuiga mfumo wa COVID-19, lakini lina uwezo wa kutosha kusoma magonjwa mengine.

Mlipuko wa mafua ya ndege katika hifadhi ya wanyama ya Delhi ulisababisha kituo hicho kufungwa kwa siku kadhaa mwezi Agosti.

Chanzo cha picha, Hindustan Times via Getty Images

Watafiti wanasema hitimisho kuu kwa watunga sera ni kwamba fursa ya kuchukua hatua ni ndogo sana kabla mlipuko haujadhibitika.

Utafiti unakadiria kuwa mara tu idadi ya maambukizi inapoongezeka kutoka mbili hadi takriban 10, kuna uwezekano mkubwa ugonjwa kusambaa zaidi ya mawasiliano ya moja kwa moja na yasiyo ya moja kwa moja.

Mawasiliano ya moja kwa moja ni watu waliokuwa na mahusiano ya karibu na ya ana kwa ana na mtu aliyeambukizwa, kama vile wanafamilia, walezi au wafanyakazi wenza wa karibu.

Mawasiliano yasiyo ya moja kwa moja ni wale ambao hawakuwa karibu moja kwa moja na mtu aliyeambukizwa, lakini waliwasiliana kwa karibu na wale waliokuwa na mawasiliano ya moja kwa moja.

Utafiti uligundua kuwa kama familia za watu waliokutana moja kwa moja ziwekwe karantini wakati kesi mbili tu zilipogunduliwa, mlipuko uweze kudhibitiwa.

Hata hivyo, kesi 10 zinapotambuliwa, kuna uwezekano mkubwa kuwa maambukizi tayari yamesambaa kwa jamii pana, na hivyo kufanya mwenendo wa mlipuko usiwe tofauti sana na hali ya awali bila hatua zozote za kuingilia kati.

Ili kuhakikisha uhalisia wa utafiti, watafiti walichagua mfano wa kijiji kimoja katika wilaya ya Namakkal, jimbo la Tamil Nadu, eneo linalojulikana kama kitovu cha ufugaji wa kuku nchini India.

Namakkal ina zaidi ya mashamba ya kuku 1,600 na takriban kuku milioni 70, na huzalisha zaidi ya mayai milioni 60 kwa siku.

Kijiji chenye wakazi 9,667 kiliundwa kwa kutumia jamii bandia inayojumuisha familia, sehemu za kazi na masoko, na kiliwekwa kwenye mazingira ya kuwasiliana na ndege waliojeruhiwa ili kuiga hali halisi ya maambukizi. Jamii bandia ni idadi ya watu inayoundwa na kompyuta ili kuiga tabia na sifa za jamii halisi.

Katika uigaji huo, virusi huanza katika eneo moja la kazi, kama shamba la ukubwa wa kati au soko la wazi, kisha husambaa kwanza kwa watu waliopo hapo (mawasiliano ya moja kwa moja), kabla ya kusambaa kwa wengine (mawasiliano yasiyo ya moja kwa moja) kupitia nyumba, shule na sehemu nyingine za kazi, ambapo mazingira haya huunda mtandao thabiti wa maambukizi.

Kwa kufuatilia maambukizi ya awali yanayohusishwa na mawasiliano ya moja kwa moja, na maambukizi ya pili yanayohusishwa na mawasiliano yasiyo ya moja kwa moja, watafiti walikadiria viashiria muhimu vya usambazaji, ikiwemo kiwango cha msingi cha uzalianaji (R0), ambacho hupima idadi ya watu ambao mtu mmoja aliyeambukizwa huwaambukiza kwa wastani.

Kwa kuwa hakukuwa na janga halisi, watafiti waliiga viwango mbalimbali vinavyowezekana vya kasi ya maambukizi.

Kisha walitazama nini hutokea hatua mbalimbali za kuingilia kati zinapotumika, kama vile kuua ndege (culling), kuwatenga watu waliokuwa na mawasiliano ya karibu, na chanjo lengwa.

Matokeo yalikuwa wazi.

Kuua ndege kulikuwa na ufanisi, lakini tu kabla binadamu hajaambukizwa na virusi.

Pindi maambukizi yanapovuka kwenda kwa binadamu, muda unakuwa jambo muhimu zaidi, watafiti waligundua.

Kuwatenga wagonjwa na kuziweka familia zao kwenye karantini kunaweza kuzuia virusi katika maambukizi ya kiwango cha pili, lakini mara maambukizi ya kiwango cha tatu, kati ya marafiki au mawasiliano ya mbali zaidi yanapoibuka, mlipuko hushindwa kudhibitiwa isipokuwa mamlaka zichukue hatua kali zaidi, ikiwemo kufunga shughuli zote (lockdown).

Chanjo lengwa husaidia kupunguza uwezo wa virusi kusambaa katika jamii kwa ujumla, lakini haipunguzi kwa kiasi kikubwa hatari ya maambukizi ya moja kwa moja ndani ya kaya.

Sekta ya kuku nchini India ni mojawapo ya sekta kubwa zaidi duniani

Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images

Pia ulionyesha tofauti ya kutatanisha.

Karantini, ikitekelezwa mapema kupita kiasi, huwafanya familia kukaa pamoja kwa muda mrefu, jambo linaloongeza uwezekano wa walioambukizwa kuwaambukiza wale wanaoishi nao. Lakini ikitekelezwa kuchelewa, haipunguzi sana kasi ya maambukizi.

Watafiti wanabainisha kuwa njia hii ina tahadhari na mapungufu kadhaa.

Mfano huo unategemea kijiji kimoja cha kubuniwa, chenye ukubwa wa kaya usiobadilika, sehemu za kazi, na mifumo maalum ya mienendo ya kila siku; haujumuishi milipuko inayoweza kutokea kwa wakati mmoja kutokana na ndege wahamiaji au mitandao ya ufugaji wa kuku, wala hauzingatii mabadiliko ya tabia, kama vile kuvaa barakoa, mara watu wanapotambua kuwa ndege wanaanza kufa.

Sima Lakdawala, mtaalamu wa masuala ya virusi katika Chuo Kikuu cha Emory, Atlanta, anaongeza tahadhari nyingine: mfano wa uigaji unadhania “usambazaji wenye ufanisi mkubwa sana wa virusi vya mafua.”

“Njia ambayo ugonjwa husambaa ni ngumu, na si kila aina (strain) ya virusi iliyo na ufanisi sawa na nyingine,” anasema Lakdawala, akiongeza kuwa wanasayansi wanaanza kutambua kuwa si kila mtu mwenye mafua ya msimu hueneza virusi kwa kiwango kilekile.

Utafiti unaoibuka unaonesha kuwa “ni sehemu ndogo tu ya watu walioambukizwa mafua wanaosambaza virusi vya mafua vinavyoambukiza hewani.”

Hali hii inafanana na jambo la kuenea kupita kiasi (super-spreading) lililoonekana wakati wa COVID-19, lakini si kali sana kwa upande wa mafua, tofauti ambayo inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa jinsi virusi vinavyosambaa katika jamii.

Nini kitatokea ikiwa virusi vya H5N1 vitaweza kuenea kati ya binadamu?

Dkt. Lakdawala anaamini kuwa “itasababisha mtikisiko mkubwa, labda zaidi kama janga la mafua ya nguruwe la mwaka 2009 kuliko COVID-19.”

“Hii ni kwa sababu tumejiandaa zaidi kwa janga la mafua, kwa kuwa tuna dawa za kuzuia virusi (antivirals) zilizoidhinishwa na zenye ufanisi dhidi ya aina za H5N1 kama ngao ya awali, pamoja na akiba ya chanjo za H5 ambazo zinaweza kutumika kwa muda mfupi,” anaeleza.

Hata hivyo, kulegeza tahadhari kutakuwa kosa. Lakdawala anaonya kuwa ikiwa H5N1 itajikita kwa binadamu, inaweza kupitia upangaji upya au kuchanganyika na aina zilizopo, jambo ambalo litaathiri zaidi afya ya umma.

Mchanganyiko huo unaweza kubadilisha muundo wa mafua ya msimu, na kusababisha milipuko ya msimu isiyotabirika na mibaya.

Watafiti wa India wanabainisha kuwa uigaji huu unaweza kuendeshwa kwa wakati halisi na kubadilishwa kadiri data mpya inavyopatikana.

Kwa kuzingatia maboresho kama kupunguza ucheleweshaji wa utoaji wa taarifa na kesi zisizo na dalili, uigaji huu unaweza kuwapa maafisa wa afya chombo muhimu sana katika saa za mwanzo za mlipuko: kuelewa hatua muhimu zaidi za kuchukua kabla dirisha la kudhibiti ugonjwa halijafungwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *