Arusha. Mkazi wa Arusha, Arafa Yusuph Matoke (74), amepata mafunzo ya Sanaa ya Upishi katika Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) cha Hoteli na Utalii kwa kipindi cha miezi mitatu.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Hussein Mohamed Omar, amemkabidhi Afara cheti cha kuwa mwanafunzi bora katika mahafali ya 13 ya chuo hicho, yaliyofanyika jana Alhamisi, Desemba 18, 2025.
Arafa ni miongoni mwa wahitimu waliopata ujuzi kupitia mpango maalumu wa kuwajengea ujuzi na maarifa kwenye vyuo vya ufundi vya Veta unaojulikana kama mwanamke na samia, ambao umewahusisha zaidi ya wanawake 16,000 kote nchini.
“Mwanzoni nilisita kujiunga na mafunzo ya muda mfupi kwa sababu nilijua sitaweza kulingana na umri wangu, lakini baada ya kuanza na wenzagu 60 walimu walinitia moyo darasani tulitumia mwezi mmoja na muda uliobaki mafunzo kwa vitendo jikoni ambako nilifanya vizuri, sasa ninaomba kazi za upishi kwenye shughuli mbalimbali,” amesema Arafa.
Dk Omar katika hotuba yake alimpongeza Arafa kwa ujasiri wake licha ya umri wake kuwa chachu kwa wengine kutumia fursa hiyo kupata ujuzi na maarifa yatakayoweza kufungua milango ya ajira na kujiajiri.
“Tatizo la ajira halipo hapa Tanzania pekee bali ni janga la dunia nzima kwasababu idadi ya wahitimu ni kubwa kuliko nafasi za ajira rasmi serikalini, kupitia chuo hiki na vyuo vingine nchini vijana mna nafasi kupata maarifa kupitia mfumo rasmi na wengine kupitia mafunzo ya muda mfupi kama alivyofanya Arafa,” amesema Dk Omar.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Veta, Anthon Kasore akimpongeza mhitimu wa kozi fupi, Arafa Yusuph Matoke (74) wakati wa mahafali ya 13 jana Desemba 18, 2025. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Hussein Mohamed Omar. Picha na Filbert Rweyemamu
Amewataka vijana nchini kutokuwa na tabia za kulalamika bali kubadilika ili kuitumia elimu waliyoipata kubadilisha maisha yao na jamii walikotoka kwa sababu ujuzi waliopata ni mtaji mkubwa ambao wakiutumia utainua viwango vya maisha yao.
“Nitoe wito kwa wahitimu hakuna Serikali inayoweza kuajiri kila mhitimu bali tutumie fursa zilizopo za ajira kwenye sekta binafsi, kujiajiri wenyewe na utaratibu wa kisheria ambao vijana kupitia vikundi wanapaswa kuchangamkia asilimia 30 ya manunuzi yote serikalini imetengwa kwa ajili ya kufanywa na makundi ya vijana,” amesema Dk Omar.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Anthon Kasore amesema mpango wa kuwapa wanawake mafunzo ya muda mfupi umelenga kuwajengea uwezo ili waendeleze shughuli zao za ujasiriamali na kuwa mwitikio umekua mkubwa tofauti na malengo ya awali.
“Veta tulikuwa na lengo la kuwapa mafunzo ya muda mfupi kupitia mpango wa wanawake na Samia, wanawake 5,000, lakini mahitaji yameongezeka hadi kuzidi 16,000 na maombi yanazidi kutufikia, elimu ya ujuzi ndio uelekeo wa kujiajiri na kuajiri wengine,” amesema Kasore.
Mkuu wa Chuo cha Hoteli na Utalii, Magu Mabelele amesema wahitimu wa kozi wanazozitoa wamekuwa wakipata elimu na ujuzi unaohitajika kutokana ushirikiano walionao na wadau wa sekta ya utalii kwa kufundisha wanafunzi wao kulingana na mahitaji ya waajiri.
Amesema wanafunzi 373 wamehitimu katika ngazi ya astashahada na stashahada kwenye kozi za sanaa ya upishi, uongozaji watalii, uhudumu na uuzaji vinywaji, uandaji wa vyumba na shughuli za usafri na utalii huku chuo hicho kikijivunia kuwa na hoteli yenye hadhi ya vyota tatu inayotumiwa na wanafunzi kwa vitendo.
Mabelele ameongeza kuwa wanaendelea kukabiliana na changamoto za uhaba wa vifaa vya kufundishia ukilinganisha na idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa hasa kwenye fani za upishi, vinywaji na utalii na kutokuwa na usafiri wa uhakika wa wanachuo wa fani ya utalii kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo.