Dar es Salaam. Uongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima, umesema unasubiri msimamo wa Serikali kuhusu upotevu na uharibifu wa mali za kanisa hilo kabla ya kuchukua hatua zaidi.
Uongozi unadai kuwepo kwa upotevu na uharibifu wa mali zenye thamani ya Sh2.7bilioni katika kipindi ambacho kanisa lao lilikuwa chini ya ulinzi wa Jeshi la polisi.
Jeshi la Polisi limesema uchunguzi dhidi ya madai hayo unaendelea kufanyiwa kazi.
“Bado uchunguzi unaendelea,” amesema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Mtatiro Kitinkwi jana Desemba 18, 2025 wakati akizungumza na Mwananchi.
Ujenzi ukiwa unaendelea katika Kanisa la Gwajima baada ya Serikali kulifungulia kuendelea na shughuli zake baada ya kusitishiwa huduma.
Novemba 25, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando aliutaka uongozi wa kanisa hilo kufanya tathimini ya mali zilizoharibiwa na kuibwa kisha kupeleka ofisini kwake kwa hatua zaidi.
Akizungumza na Mwananchi jana, mchungaji kiongozi na mkuu wa utawala na fedha wa makanisa ya Ufufuo na Uzima, Askofu Baraka Tegge amesema tayari wamewasilisha tathimini ya uharibifu na upotevu wa mali kwenye ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Ubungo.
“Tunachokisubiri ni majibu yao kuhusu uharibifu na upotevu huo, ili tujue nini tufanye, majibu yao ndiyo yatatupa mwelekeo wa jambo hili, kama tuchukue hatua zaidi au vinginevyo,” amesema.
Desemba 16, 2025 Mwananchi ilipomtafuta Msando kueleza kama ofisi yake imepokea ripoti ya uharibifu na hatua gani imeanza kuchukulia, lakini aliomba atafutwe wakati mwingine kuzungumzia hilo.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima. Picha na Mtandao
Msando alipotafutwa tena, Desemba 18 na 19 kuzungumzia hatua inayochukuliwa na Serikali kutokana na upotevu wa mali za kanisa hilo simu yake iliita bila kupokewa.
Awali, kanisa hilo lilifutiwa usajili wa kuendelea na huduma tangu Juni 2, 2025 kwa kile kilichoelezwa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa kuwa limekiuka Sheria za Usajili Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa.
Katika barua yake kwa Askofu Gwajima, Kihampa alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya askofu huyo kuonekana akitoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa kupitia mimbari ya kanisa hilo, akielezwa kuwa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.
Baadaye, Gwajima alitoka hadharani na kukanusha taarifa za kanisa lake kufungwa akisema kwenye mitandao watu wanapitisha karatasi kwamba Kanisa la Ufufuo na Uzima limefungwa, “hakuna wa kufunga kanisa la Mungu duniani, si kweli, ni uongo, ni wahuni.”
Waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima wakiwa katika ibada ya kwanza ya Jumapili Novemba 30, 2025 baada ya kanisa hilo kufunguliwa. Picha na Maktaba
Hata hivyo, kupitia video iliyochapishwa katika mitandao ya kijamii, Gwajima akiwa na viongozi wengine wa Kikristo, alisema kuwa polisi wamezingira kanisa lake, baada ya barua juu ya kufungwa kwa kanisa hilo.
Hadi Novemba 25, 2025 saa 7:30 mchana kanisa hilo lilikuwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi.
Novemba 24, 2025 Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba alitangaza kanisa hilo lifunguliwe na siku sita baada ya agizo hilo msimamo mwingine wa Serikali ukatolewa mpango wa kutafutwa au kukamatwa kwa kiongozi huyo ukome.
Baada ya maagizo hayo, Novemba 30, 2025 waumini walifanya ibada ya kwanza ya Jumapili, ikiwa imepita takribani miezi sita tangu kufutiwa usajili, Askofu Tegge alieleza uharibifu wa mali za kanisa uliofanyika katika kipindi ambacho lilikuwa chini ya ulinzi wa polisi.
Alidai mali zenye ya Sh2.7 bilioni zimeibwa na kuharibiwa ikiwamo fedha taslimu Sh420 milioni zilizokuwa zimewekwa kwenye shelfu maalumu.
Vingine alivyovitaja ni vifaa vya kanisa pamoja sare za wanakwaya akibainisha kuwa, kwenye ofisi ya utawala, laptop yenye nyaraka za ofisi na taarifa nyingine pamoja na runinga vyote vimeibiwa.
Magari ya Polisi yakiwa nje ya Kanisa la Ufufuo na Uzima wakati lilipofungwa. Picha na Maktaba
Vingine alivyovitaja ni nakala za vyeti za ndoa, vyeti vya ubatizo huku ofisi ya askofu mkuu ikivunjwa na mali zilizoibwa katika ofisi hiyo ni computer printer, TV na Ipad.
Pia, kwenye ofisi ya machapisho mali zilizoibwa ni kompyuta, nyaraka, hard disk na printer wakati kwenye stoo ya kanisa zilizoibwa ni sare za wanakwaya vyombo vya kupikia, masufuria, sahani na vikombe.
Alidai kwenye ukumbi wa kanisa, mali zilizoibwa ni viti 1,826, mixer ya kanisa, waya microphones, spika na Digital amplifier.
Wakati kwenye stoo yakutunzia vifaa vya muziki vyote vimechukuliwa ikiwamo mixer, extension cable na spika kubwa.
“Kwenye chumba cha printing mali zilizoibiwa ni laptop, kompyuta aina ya iMac na vifaa vya kuprinti, milango ya kanisa nayo imeharibiwa. Thamani ya mali zote ni Sh2.76 bilioni,” amesema.
Leo Ijumaa Desemba 19, Mwananchi imetembelea Makao Makuu ya Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Kimara jijini Dar es Salaam na kukuta ukarabati na ujenzi wa kanisa hilo ukiendelea.
Mmoja wa waumini ambaye alikutwa kanisani hapo kwa masharti ya kutotajwa jina lake ameeleza kuwa ujenzi huo ulianza kabla ya kanisa kufungwa, hivyo kinachofanyika sasa ni mwendelezo tu.
“Kinachofanyika hapa si jambo jipya, ujenzi ulikuwa unaendelea kabla hatujafungiwa na mafundi waliondolewa bada ya tangazo lile kanisa kufungwa,” amesema.