NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew amezitaka Bodi za Mabonde ya Maji nchini kufanya tathmini ya kina ya vyanzo vyote vya maji ili kubaini hali yake.

Amesema itahusu kujua uhalisia, ikiwemo uvamizi, uharibifu na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema hayo akiwa katika ziara mkoani Songwe akikagua utekelezaji wa miradi ya maji inayotekelezwa na serikali ili kuwahudumia wananchi.

Kundo ameongeza kuwa tathmini hiyo itasaidia kujua ni vyanzo vipi vinaendelea kufanya kazi, vipi vimedhoofika na vipi vimekauka, hatua itakayoiwezesha serikali kuwa na takwimu sahihi za kupanga mipango ya sasa na ya baadaye.

SOMA: Rais Samia aagiza vyanzo vya maji kutuzwa

Amebainisha kuwa vyanzo vya maji havikauki ghafla bali huonesha dalili na mwenendo, hivyo ni muhimu serikali kuwa na mfumo wa kisasa wa taarifa (database) unaosasishwa mara kwa mara ili kufuatilia mwenendo wa kila chanzo.

Ameagiza kubainishwa na kuibuliwa kwa vyanzo vipya vya maji ili kuwa na vyanzo mbadala, akisisitiza kuwa maandalizi ya miradi mipya yafanyike mapema kabla vyanzo vya awali havijakauka kabisa.

Hatua hizo zitawezesha Serikali kupanga vizuri usimamizi, ulinzi na uendelezaji wa vyanzo vya maji, kuongeza upatikanaji wa maji safi kwa wananchi na kuboresha elimu kwa umma kuhusu uhifadhi wa rasilimali za maji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *