BEKI wa zamani wa Coastal Union na Simba, Abdi Banda anayekipiga kwa sasa Dodoma Jiji, ameshindwa kujizuia na kuweka bayana kinachoigharimu timu katika Ligi Kuu, huku akichekelea kupatikana kwa vibali vya wachezaji wa kigeni waliosajiliwa na timu hiyo bila kutumika.

Banda, mtoto wa beki wa kati na nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Hassan Banda aliyewahi kutamba na African Sports, Simba na Taifa Stars, ameweka wazi kilichoiponza Dodoma Jiji ni kuwakosa baadhi ya mastaa, lakini anashukuru mambo yamekaa sawa.

Dodoma ipo nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi sita tu baada ya mechi nane, ikishinda moja kuitoka sare tatu na kupoteza nne na Banda amesema bado haijawakatisha tamaa kwa vile wanaamini mastaa wao wa kigeni waliokuwa wamekwama kwa sababu ya vibali wataiongezea nguvu Dodoma Jiji.

BAND 01

Akizungumza na Mwanaspoti, Banda amesema timu ilipunguzwa makali kwa kukosekana kwa mastaa wa kigeni waliosajiliwa dirisha kubwa ambao hawakuwa na vibali ila kwa sasa kwa mujibu wa mabosi ni kwamba kila kitu kipo sawa na watatumika Ligi Kuu ikirejea mwishoni mwa Januari mwakani.

Banda Amesema hawezi kupingana na ugumu wa ligi ambao umekuwa changamoto kubwa kwa mastaa hao kwani timu nyingi zinaonekana kujipanga msimu huu.

“Ligi ni ngumu na zile pointi za Pamba Jiji tulizonyang’anywa ndio zimetufanya tuwe hapa ila kikubwa tunazidi kupambana ili kupunguza makosa.”

 “Wachezaji wetu wa kigeni wamepata vibali, kwa hiyo tutakaporejea basi kutakuwa sapraizi kwani tutakuwa tumekamilika sasa.”

BAND 02

“Tumeanza mazoezi wiki hii na sababu iliyomfanya kocha aanze kutunoa mapema ni maandalizi ya kutufanya tuwe timamu kabla mechi hazijaanza, kwani tutakuwa na mechi mfululizo,” amesema Banda mwenye asisti mbili hadi sasa katika ligi hiyo.

Dodoma Jiji inajiandaa karibu kwa karibu mwezi mzima kabla ya kukukabiliana na Tanzania Prisons kwenye mechi itakayopigwa Januari 22 mwakani kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *