Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amekosolewa vikali kufuatia kauli yake kuhusu maandalizi ya kuwapa askari polisi na wanajeshi risasi 120 kila mmoja kwa ajili ya kukabiliana na vurugu wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Januari mwakani. Kauli hiyo imeibua mjadala mpana ndani na nje ya nchi kuhusu usalama, demokrasia na haki za binadamu.
Museveni alitoa matamshi hayo wakati akijibu swali la mwanahabari katika moja ya vikao vya jioni vya kampeni zake. Swali hilo lilihusu mwito wa mara kwa mara wa mpinzani wake mkuu, Robert Kyagulanyi, anayejulikana kama Bobi Wine, anayewahimiza wapigakura kubaki kwenye vituo vya kupigia kura ili kuhakikisha kura zao haziibiwi.
Akijibu, rais Museveni ambaye ni mgombea wa chama tawala cha NRM, alisema kuwa askari wa usalama wako tayari kukabiliana na vurugu zozote, akitaja idadi ya risasi walizonazo kama ishara ya nguvu ya dola.
“Nimekuwa nikimsikia Kyagulanyi akisema askari ni wachache na wanaoweza kufanya vurugu ni wengi. Msimsikilize, kwa sababu kila askari ana risasi 120. Mkisema wanaofanya vurugu ni wengi, walingenisheni na idadi ya risasi za askari,” alisema Museveni.
Kauli hiyo imeibua hofu na wasiwasi miongoni mwa wananchi wengi, huku baadhi wakisema matamshi hayo yanaweza kuwakatisha tamaa raia kujitokeza kupiga kura. Wengine wameeleza kuwa amani na uthabiti wa taifa haviwezi kudumishwa kwa vitisho vya silaha.
Huwezi kuahidi amani kwa bunduki na risasi
Baadhi ya wananchi wamekosoa mtazamo huo wakisema kuwa historia ya dunia inaonyesha kuwa nguvu za kijeshi haziwezi kuzima sauti ya watu kwa muda mrefu.
“Huahidi amani kwa watu kwa kuwaambia una risasi na bunduki. Hapajawahi kutokea vita duniani ambapo watu wengi wanaopinga jambo hushindwa kwa bunduki,” alisema mmoja wa wananchi.
Kwa upande wake, mgombea wa chama kikuu cha upinzani cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi, amemshtumu vikali rais Museveni kwa kauli hiyo, akisema ni ya kutisha na inayokiuka misingi ya haki za binadamu.
Kyagulanyi aliwahimiza polisi na wanajeshi kutokubali kutumiwa kuwaua wananchi wenzao wanaotekeleza haki zao za kikatiba wakati wa uchaguzi.
“Ujumbe wangu kwa polisi na wanajeshi: huyu bwana amezeeka na anaondoka. Nyinyi mnajua kuwa kwa mujibu wa sheria za haki za binadamu, mtawajibika binafsi kwa vitendo vyovyote vinavyokiuka haki za binadamu,” alisema Kyagulanyi.
Aliongeza kuwa wananchi ambao Museveni anawataja kama wahusika wa vurugu ni ndugu, dada, jamaa na Watanzania wenzao—akisisitiza kuwa ni raia wa Uganda wanaotumia haki yao ya kisheria.
Mkuu wa majeshi ajiingiza moja kwa moja kwenye mjadala wa uchaguzi
Mjadala kuhusu iwapo wapigakura waruhusiwe kubaki kwenye vituo vya kupigia kura kusubiri matokeo umeendelea kushika kasi ndani na nje ya Bunge la Uganda. Mjadala huo uliongezeka baada ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mwana wa rais Museveni, kutoa onyo kali kuhusu suala hilo.
Hata wiki hii, wakati wa sherehe za kuvisha maafisa wa jeshi nyota, Jenerali Kainerugaba alirudia onyo hilo akisema kuwa wananchi wanapaswa kupiga kura na kurejea nyumbani mara moja bila kubaki kwenye vituo vya kupigia kura.
“Tunatoa mwito kwa wananchi kupiga kura kwa amani na waende nyumbani. Wasibaki kwenye vituo vya kupigia kura. Watakaojaribu kuzusha vurugu tutachukua hatua za haraka kwa kutumia zana zozote tulizo nazo,” alisema.
Uchaguzi mkuu wa Uganda unatarajiwa kufanyika tarehe 15 Januari mwakani, huku wagombea wanane wa urais wakiendelea na kampeni zao katika maeneo mbalimbali ya nchi. Watazamaji wa siasa za Uganda na mashirika ya haki za binadamu wanaendelea kufuatilia kwa karibu mazingira ya uchaguzi huo.
