
Tangu mwanzoni mwa mwezi Desemba, Burundi imekuwa ikikabiliwa na wimbi jipya kubwa la wakimbizi kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Kulingana na ripoti ya mashirika mbalimbali iliyoratibiwa na Umoja wa Mataifa, karibu watu 90,000 wamevuka mpaka wa Burundi katika kipindi cha chini ya wiki mbili wakikimbia vurugu huko Kivu Kusini, haswa Uvira na maeneo yanayoizunguka.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kutokana na ukubwa wa mgogoro huo, mashirika na washirika hawa wa Umoja wa Mataifa walitoa wito mpya siku ya Jumatano, Desemba 17, ya dola milioni 33.2 ili kufadhili mwitikio wa dharura.
Katika “wito wao wa mwitikio wa Dharura wa mashirika mbalimbali kwa wakimbizi nchini Burundi,” mashirika manane ya Umoja wa Mataifa na washirika kati ya mashirika hayo yanasema kwamba dola milioni 33.2 zitatumika kugharamia mahitaji ya msingi ya familia 16,000 ambazo zimewasili katika siku kumi zilizopita kutoka mashariki mwa DRC. Watu hawa wako katika hali ya mbaya sana.
Mashirika ya kibinadamu yataweza kukabiliana na mgogoro huo hadi mwezi Machi na kushughulikia ukosefu wa makazi, chakula, vyoo, na dawa.
Vipaumbele vinne vimefafanuliwa. Kwanza, kuhakikisha ulinzi wa raia, kwa mujibu wa kanuni ya kutowafukuza wakimbizi. Pili, kuhakikisha upatikanaji wa mahitaji ya msingi, kwa sababu kutokana na msongamano wa wakimbizi, wakimbizi wanaishi katika mazingira yasiyo safi. Pia wanataka kuimarisha uratibu na uhamasishaji wa rasilimali.
Lakini moja ya vipaumbele muhimu ni maendeleo ya haraka ya eneo la Bweru. Eneo hili limetengwa na mamlaka ya Burundi kama eneo la kipaumbele la kuhamishiwa wakimbizi hawa ili kupunguza shinikizo kwenye mpaka.
Karibu watu 13,000 tayari wamehamishiwa huko. Hata hivyo, miundombinu iliyopo haitoshi, hasa katika suala la upatikanaji wa barabara, vituo vya maji, vyoo, na makazi ya dharura.
Katika wito wake, Umoja wa Mataifa unaelezea dharura ya kibinadamu ambayo inaongeza shinikizo kwa Burundi. Hii inakuja wakati nchi hiyo inapitia mgogoro mkubwa wa kijamii na kiuchumi na tayari ilikuwa ikiwapa hifadhi, kabla ya mwezi Desemba, wakimbizi wapatao 90,000 wa Kongo na watafuta hifadhi 2,000.