Mkutano na waandishi wa habari wa Rais Vladimir Putin umeanza kwa hoja zilezile anazotumia mara kwa mara kuhalalisha vita dhidi ya Ukraine.

Ametaja tena kile anachokiita “mapinduzi” ya mwaka 2014, yaliyomwondoa madarakani rais mwenye mwelekeo wa Urusi, Viktor Yanukovych, na kuishutumu Ukraine kwa madai ya “kuchochea vita”.

Kwa mujibu wa rais Putin, matukio hayo ndiyo chanzo cha hali ya sasa ya mgogoro.

Putin pia amesema kuwa Ukraine “inakataa kumaliza mgogoro huu kwa njia za amani” na haiko tayari kujadili masuala ya mipaka au kutoa ardhi.

“Chanzo kilichosababisha mgogoro huu lazima kishughulikiwe”, akionesha tena kutokuwa tayari kufanya maridhiano.

Kauli hii inaashiria msimamo wa Urusi kwamba sababu ilizotaja ndizo zilizochangia uvamizi wa kijeshi mwaka 2022.

Rais huyo wa Urusi anafanya mkutano wake wa mwisho wa mwaka kwa njia ya simu na waandishi wa habari.

Tukio la mwaka huu litakuwa na mseto wa mambo ambapo Putin atajibu maswali ya waandishi wa habari, pamoja na maswali yaliyowasilishwa na umma kwa ujumla katika wiki za hivi karibuni.

Kremlin imesema karibu maswali milioni tatu yalitumwa katika ofisi ya rais Putin na kwamba yote yameshughulikiwa kwa karibu.

BBC imepiga kambi katika ukumbi ambapo tukio hilo litafanyika karibu na Kremlin.

Wafanyakazi wengi wa televisheni za nchini Urusi wanaonekana wakifanya matangazo ya moja kwa moja.

Kwa Vladimir Putin inatoa nafasi ya kutangaza mtazamo wake kwa ulimwengu na kujipambanua kama baba wa taifa anayetatua matatizo ya Warusi (zaidi ya watu milioni mbili wametuma maswali kwa kiongozi wa Kremlin).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *