Ufilisi wa biashara Ujerumani wapanda kwa miaka 11Ufilisi wa biashara Ujerumani wapanda kwa miaka 11

Takwimu za robo tatu za kwanza za mwaka 2025 zinaonyesha kuwa biashara ndogo ndogo nchini Ujerumani ndizo zilizoathirika zaidi na mdororo wa uchumi uliodumu kwa karibu miaka mitatu katika uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya.

Mnamo Desemba 12, mchambuzi mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Biashara na Viwanda la Ujerumani (DIHK), Volker Treier, aliiambia shirika la habari la Reuters kuwa “wimbi la kufilisika kwa biashara linaendelea.” Aliongeza kuwa biashara ndogo na za kati ndizo zinazokumbana zaidi na changamoto.

Katika utafiti wa hivi karibuni, DIHK ilibaini kuwa karibu kampuni moja kati ya tatu zenye wafanyakazi chini ya 20 zinatarajia hali ya biashara zao kuzorota zaidi. Biashara za aina hii zinachangia takribani asilimia 85 ya biashara zote nchini Ujerumani.

Takwimu rasmi zimethibitisha mwenendo huo, ambapo Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Ujerumani (Destatis) ilitangaza siku hiyo hiyo kuwa mahakama za ndani zilisajili kesi 18,125 za kufilisika kwa kampuni hadi mwisho wa Septemba. Idadi hiyo ni karibu ongezeko la asilimia 12 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Hali hiyo imefanya idadi ya kampuni zilizofilisika katika robo tatu za kwanza za mwaka 2025 kuwa kubwa zaidi tangu mwaka 2014.

Biashara ndogo ndizo zilizo hatarini zaidi

Watafiti wa masuala ya ufilisi wanasema haishangazi kuona biashara ndogo ndogo zikiathirika zaidi na uchumi unaosuasua.

Steffen Müller, mkuu wa utafiti wa ufilisi katika Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi ya Halle (IWH), anasema wimbi la hivi karibuni la kufilisika “linajitokeza zaidi katika biashara ndogo.”

Akizungumza na DW, Müller alisema kampuni nyingi zilizofilisika zilikuwa na wastani wa wafanyakazi 10, huku akiongeza kuwa nyingi zilikuwa ndogo zaidi ya hapo.

Ujerumani | Kundi la KaDeWe latangaza kufilisika
Mnamo Januari 28, 2024, duka maarufu la Kaufhaus des Westens (KaDeWe), ambalo ni sehemu ya Kundi la makampuni ya Signa lilikuwa karibu kufilisika, hali iliyotia doa moja ya alama maarufu zaidi za biashara ya rejareja mjini Berlin.Picha: Michael Kuenne/ZUMAPRESS/picture alliance

Msukosuko wa kifedha unaonekana pia nje ya sekta ya biashara. Idadi ya watu wanaofilisika binafsi imeongezeka tena mwaka huu, ambapo kesi 57,824 za ufilisi wa walaji zilirekodiwa katika robo tatu za kwanza za mwaka, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 8 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Shinikizo linaongezeka kwa ajira

Ingawa biashara nyingi zinazofilisika ni ndogo, ongezeko hilo pia limesababisha kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya ajira zilizopotea au zilizo hatarini. Kulingana na makadirio ya Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi ya Halle (IWH), takribani ajira 170,000 zimeathiriwa mwaka huu, ikilinganishwa na chini ya ajira 100,000 kabla ya janga la UVIKO-19.

Klaus-Heiner Röhl, mchumi kutoka Taasisi ya Kiuchumi ya Ujerumani (IW) mjini Cologne, anaonya dhidi ya kuiongeza kupita kiasi athari ya hali hiyo kwa ajira. Akizungumza na DW alisema kuwa kufilisika kwa biashara huchangia ongezeko dogo la ukosefu wa ajira, lakini hali si mbaya sana.

Hata hivyo, mtafiti wa IWH, Steffen Müller, anaona athari kwa soko la ajira zitakuwa kubwa zaidi. Makadirio yake yanaonyesha kuwa karibu ajira 200,000 zitaathiriwa mwaka 2025, ikiwa ni karibu mara mbili ya kiwango kilichokuwapo kabla ya janga.

Aliongeza kuwa baadhi ya ajira hizo huenda zikapotea kabisa kwa sababu kufilisika kwa biashara kunasababisha baadhi ya kampuni kufungwa.

Hata hivyo, Müller anasisitiza kuwa kwa ujumla hali bado inadhibitika, kwani ajira mpya mara nyingi hujitokeza katika kampuni nyingine, na wafanyakazi huhamia kutoka biashara dhaifu kwenda zilizo imara zaidi wakati wa mabadiliko ya soko.

Ufilisi nchini Ujerumani
Kiwango cha ufilisi wa makampuni nchini Ujerumani kimekuwa cha juu zaidi katika muda wa miaka 10 iliyopitaPicha: Oliver Boehmer/Zoonar/picture alliance

Je, hali hii ilitarajiwa?

Wachumi wote wawili wanasema ongezeko la kufilisika kwa biashara lilitarajiwa kwa kiasi kikubwa. Müller alisema kuwa ongezeko hilo lilionekana mapema, ingawa ukubwa wa ongezeko hilo ulikuwa wa kushangaza kidogo.

Röhl naye anakubaliana, akieleza kuwa uchumi wa Ujerumani umekuwa ukidorora kwa muda mrefu. Alisema kuwa kutokana na udhaifu unaoendelea wa uchumi, idadi ya biashara zilizofilisika ingeweza kuwa kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa.

Röhl anaeleza kuwa sababu kuu ya hali hiyo ni mambo ya jumla ya uchumi, akitaja karibu miaka mitatu ya uzalishaji wa kiuchumi kusimama au kushuka kidogo. Aidha, bei kubwa za nishati, vita vya Urusi nchini Ukraine, pamoja na mpito kuelekea uchumi usioathiri mazingira, vimeongeza mzigo wa kifedha kwa kampuni nyingi.

Hata hivyo, Röhl anaongeza kuwa ni vigumu kupima kwa usahihi ni kwa kiwango gani kuchelewa kwa mageuzi ya sera au hatua za marekebisho ndani ya kampuni kumechangia tatizo hilo.

Kwa upande wake, Müller anakataa kulaumu sababu moja pekee. Anasema sababu za kufilisika hutofautiana kwa kila kampuni, akitaja mambo kama maamuzi mabaya ya bidhaa, migogoro ya kiusimamizi au kutofautiana na wadau muhimu. Anasema matatizo haya yanapokutana na gharama zinazoongezeka, mabadiliko ya kimuundo, hali ya kutokuwa na uhakika wa kisiasa kimataifa na ushuru, kufilisika hutokea kwa haraka zaidi.

Müller anasisitiza kuwa ni nadra kwa kampuni imara na yenye ushindani kufilisika kwa sababu ya hali mbaya ya nje pekee.

Ushuru wa Marekani watishia wazalishaji mvinyo Ujerumani

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Dalili chache za nafuu

Shirikisho la Wasimamizi na Wadhamini wa Ufilisi nchini Ujerumani (VID) limeonesha matumaini ya tahadhari kuhusu hali inayoendelea.

Akizungumza na shirika la habari la Ujerumani dpa hivi karibuni, mwenyekiti wa VID, Christoph Niering, alisema kuwa baada ya athari za janga la UVIKO-19 na ongezeko la kufilisika lililotokana nalo, hali inaanza kurejea katika mwenendo wa kawaida. Hata hivyo alisisitiza kuwa bado si mabadiliko makubwa, bali “kuna mwanga wa matumaini.”

Kwa upande wake, Müller anatarajia idadi ya biashara zitakazofilisika mwaka 2026 kubaki karibu na viwango vya juu vilivyoonekana mwaka huu.

Alisema hali hiyo ni habari njema kwa sehemu tu, akionya kuwa Ujerumani imeingia katika “eneo hatarishi.” Anaeleza kuwa hali haitazidi kuwa mbaya zaidi kwa kiasi kikubwa, kwani kwa kampuni kubwa, viwango vya ufilisi vinafanana na vile vilivyokuwapo takribani miaka 20 iliyopita.

Naye Röhl anaona uwezekano wa hali kupungua makali katika kipindi kijacho. Ikiwa uchumi wa Ujerumani utakua kwa takribani asilimia moja mwaka ujao, kama inavyotabiriwa na taasisi kadhaa za utafiti, anaamini shughuli za ufilisi zitapungua pia.

Hata hivyo, Röhl anaonya kuwa changamoto za kimuundo zitaendelea kuwepo, akitaja ushuru wa Marekani, ushindani kutoka China, pamoja na gharama kubwa za nishati ambazo bado ni kikwazo kwa biashara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *