UN yahimiza msaada kwa wakimbizi wa DRC nchini BurundiUN yahimiza msaada kwa wakimbizi wa DRC nchini Burundi

Umoja wa Mataifa umeomba ufadhili wa dharura wa dola milioni 33.2 kusaidia zaidi ya watu 80,000 waliokimbilia Burundi kufuatia mashambulizi mapya ya waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). 

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, wimbi hilo jipya la wakimbizi lilianza baada ya waasi wa M23 kuzidisha mashambulizi yao mapema mwezi Desemba karibu na mpaka wa Burundi, licha ya Rwanda na DRC kusaini makubaliano ya amani mjini Washington.

Awali, waasi hao waliteka miji mikubwa ya Goma mwezi Januari na Bukavu mwezi Februari, kabla ya kuendeleza mashambulizi kuelekea kusini mwa mkoa wa South Kivu. Tarehe 10 Desemba, M23 walichukua udhibiti wa mji wa Uvira, wenye mamia ya maelfu ya wakaazi, hatua iliyowapa udhibiti wa mpaka wa ardhini kati ya DRC na Burundi.

Chini ya shinikizo la Marekani, M23 walitangaza kuwa wangejiondoa Uvira. Hata hivyo, vyanzo vya usalama na wakazi wa eneo hilo vinasema baadhi ya askari wa kundi hilo, wakiwemo maafisa wa polisi na ujasusi, waliendelea kuonekana mjini humo siku ya Alhamisi.

Rwanda Rusizi 2025 | Wakimbizi wa Kongo walioko kambi ya Rusizi
Wakongo walisimulia visa vya mauaji ya kutisha dhidi ya majirani zao na kupoteza watoto katika machafuko wakati wakirotoka mauaji nchini mwao.Picha: Vivien Latour/AFP

Maelfu ya wakimbizi waingia Burundi

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi (UNHCR) ilisema kuwa mapigano makali, hasa karibu na Uvira, yamesababisha kuingia kwa wakimbizi wapatao 80,000 nchini Burundi tangu Desemba 5 kupitia vituo mbalimbali vya mpakani.

Kati ya wakimbizi hao, 71,989 ni raia wa Congo, huku takribani 8,000 wakiwa raia wa Burundi waliorejea nchini kwao wakikimbia ghasia. UNHCR inakadiria kuwa idadi ya wakimbizi wapya inaweza kufikia 90,000 katika siku zijazo.

Kutokana na hali hiyo, Umoja wa Mataifa ulizindua ombi la ufadhili wa dola milioni 33.2 ili kuwezesha wakimbizi hao kupokelewa katika mazingira yenye heshima, yakijumuisha makazi, chakula, huduma za afya na ulinzi. Shirika hilo lilichapisha pia picha zinazoonesha wakimbizi wakilazimika kulala chini ya miti bila miundombinu yoyote ya msingi.

Awali wiki hii, maafisa wawili wa Burundi walikadiria kuwa takribani watu 85,000 wamekimbia DRC katika wiki za hivi karibuni na kutafuta hifadhi nchini Burundi.

Rais wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati (ECCAS), Ezechiel Nibigira, alisema kuwa wakimbizi 25,000 wako katika eneo la Gatumba, magharibi mwa Burundi, huku karibu 40,000 wakiwa Buganda, kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo, wengi wao wakiwa hawana mahitaji ya msingi kabisa.

M23 yaonya huenda ikatanua udhibiti hadi Katanga

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Katika mji wa kusini-magharibi wa Rumonge, msimamizi wa eneo hilo, Augustin Minani, alielezea hali kuwa “ya janga”, akisema kuna wakimbizi kati ya 20,000 hadi 25,000 kutoka DRC ambao wanakosa kila kitu, huku wengi wao wakikabiliwa na njaa kali.

Umoja wa Mataifa pia uliripoti kuwa zaidi ya watu 200,000 walikimbia makazi yao wiki iliyopita kutokana na mashambulizi ya M23, ingawa bado haijabainika ni wangapi kati yao wameingia Burundi.

Burundi nayo yazindua mpango wake wa wakimbizi

Katika hatua nyingine, Burundi ilizindua mpango wa dharura wa kibinadamu tarehe 17 Desemba 2025 ili kukabiliana na ongezeko kubwa la wakimbizi. 

Waziri wa Mambo ya Ndani, Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Umma, Léonidas Ndaruzaniye, alisema kambi kama Musenyi zimezidiwa uwezo, huku wakimbizi 76,015 wakisajiliwa na wengine 12,786 kuhamishiwa Busama, mkoani Ruyigi, kupunguza msongamano.

Vita vyarindima Kongo licha ya mkataba wa Trump

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Akizungumza na waandishi wa habari, Ndaruzaniye alisema mpango huo wa dharura unalenga kutoa makazi, chakula, huduma za afya na usalama, huku ukiisaidia serikali kulinda na kuwahudumia zaidi ya wakimbizi 110,000 waliopo tayari nchini, pamoja na takribani 100,000 wanaotarajiwa kuwasili.

Wakati huo huo, mapigano yanaendelea kila siku katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, huku serikali ya Kongo ikitupilia mbali ahadi ya M23 kujiondoa, ikidai ni hila ya kisiasa. Rwanda imekanusha madai ya kuunga mkono waasi hao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *