Dar es Salaam. Kampuni ya Raddy Energy Solution Limited ya Tanzania imeingia mkataba wa kununua mitambo minne ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia kutoka kampuni ya Siemens Energy ya Uswidi kwa thamani ya dola za Marekani milioni 320 (zaidi ya Sh320 bilioni).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Desemba 19,2025 na Ubalozi wa Tanzania nchini Uswidi, mradi huo unaotarajiwa kuongeza megawati 177 kwenye gridi ya umeme nchini huku nategemeo ya kuwasili na kufungwa kwa mitano hiyo nchini ni mwishoni mwa 2027.
Ununuzi wa mitambo hiyo umewezeshwa na Benki ya CRDB kama mshirika wa ndani, kwa kushirikiana na taasisi za fedha za Serikali ya Uswidi.
“Raddy Energy ni kampuni dada kiwanda cha Raddy Fibers kilichopo Mkuranga, mkoani Pwani. Mradi huo unaelezwa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kampuni hiyo kuongeza uzalishaji wa umeme nchini, ikiwa ni hatua ya awali kuelekea lengo la kufikisha megawati 1,000 ifikapo mwaka 2030,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya ubalozi, katika utekelezaji wa mradi huo, CRDB itafanya kazi kwa karibu na taasisi za Serikali ya Uswidi, zikiwemo Wakala wa Mikopo ya Mauzo ya Nje wa Uswidi (EKN).
Taasisi zingine ni Shirika la Mikopo ya Mauzo ya Nje la Uswidi (SEK), Taasisi ya Fedha za Maendeleo ya Uswidi (Swedfund), Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Uswidi (SIDA) pamoja na Taasisi ya Mauzo ya Nje na Uwekezaji ya Uswidi (Business Sweden).
Vilevile, Baraza la Kimataifa la Viwanda la Uswidi (NIR) nalo litashiriki kutoa ushauri wa kitaalamu kwa timu ya kimataifa itakayotekeleza mradi huo.
Kikao cha pamoja baina ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uswidi, kampuni ya Raddy Energy, Benki ya CRDB na wawakilishi wa taasisi za fedha za Serikali ya Uswidi wakiendelea na kikao jijini Stockholm, hivi karibuni.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa kati ya Desemba 10 hadi 13, 2025, watendaji wa Raddy Energy walifanya ziara ya kimkakati nchini Uswidi, chini ya uratibu wa Ubalozi wa Tanzania, ambapo walikutana na uongozi wa Siemens Energy na taasisi za fedha za Serikali ya Uswidi.
Kikao kilifanyika katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje jijini Stockholm, kabla ya kutembelea makao makuu ya Siemens mjini Finspång.
Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Uswidi, Mobhare Matinyi,Raddy Energy ikiwakilishwa na Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji, Ramadhan Hassan Mlanzi na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara na Miradi, Ediphine Masase.
Kwa upande wa Benki ya CRDB, timu ya miradi mikubwa iliongozwa na Bw. Musa Lwila, akishirikiana na Saidi Salehe na Bw. Andrew Mbunda.
Siemens Energy iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Ufadhili wa Miradi, Joakim Tornberg na Meneja Mwandamizi wa Mauzo, Christiane Carlsson.
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Matinyi amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Uswidi unaendelea kuimarika, akibainisha kuwa Tanzania ina fursa kubwa za biashara na uwekezaji katika sekta za nishati, madini, viwanda, kilimo cha biashara, usafirishaji, utalii pamoja na teknolojia na ubunifu.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini, kuhimiza ukuaji wa viwanda na kufungua fursa za Tanzania kuuza umeme nje ya nchi katika miaka ijayo.