Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amerejelea utayari wa Jamhuri ya Kiislamu kushiriki mazungumzo yanaliyojengwa juu ya heshima kwa haki za taifa, huku akipinga vikali mbinu zozote zinazotegemea shinikizo la upande mmoja.

Abbas Araghchi alitoa kauli hiyo katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Yvette Cooper, siku ya Ijumaa. Araghchi alikosoa mtazamo usio na uwajibikaji wa nchi tatu za Ulaya yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, kuhusu mpango wa nyuklia wa amani wa Iran.

Amesema Jamhuri ya Kiislamu haijawahi kukataa mazungumzo iwapo yamejengwa juu ya heshima kwa haki halali na maslahi ya taifa la Iran. Hata hivyo, alibainisha kuwa Tehran haitakubali mazungumzo yanayogeuka kuwa mashinikizo ya upande mmoja.

Mazungumzo hayo yalijiri katikati ya mvutano uliozidi baada ya hatua isiyo halali ya nchi tatu za Ulaya dhidi ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, maarufu kama JCPOA. Mnamo Agosti 28, troika hiyo ilitumia kifungu kinachoitwa “snapback” chini ya JCPOA, hatua iliyozindua mchakato  wa kurejesha vikwazo vyote vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.

Tehran ilipinga  hatua hiyo na kuitaja kuwa isiyo halali, ikieleza kuwa Marekani ilijiondoa kwa upande mmoja kwenye makubaliano hayo mwaka 2018, na kwamba nchi tatu za Ulaya zimejipanga sambamba na vikwazo visivyo halali vilivyorejeshwa baada ya kujiondoa kwa Washington. Iran ilisisitiza kuwa badala ya kufuata mkondo wa Marekani, mataifa hayo yalipaswa kutekeleza wajibu wao chini ya makubaliano.

Juhudi za Russia na China katika Baraza la Usalama mnamo Septemba 26 za kutoa muda zaidi kwa diplomasia hazikupata uungwaji mkono wa kutosha. Baada ya siku mbili, washirika wa Magharibi walidai kuwa maazimio ya awali ya Umoja wa Mataifa na vikwazo husika dhidi ya Iran vimewekwa tena, wakizitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutekeleza hatua hizo za shinikizo.

Katika mazungumzo hayo, Cooper alisisitiza “ulazima” wa kuendeleza diplomasia kuhusiana na shughuli za nyuklia za Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *