
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amelaani kuongezeka kwa mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni wasiokuwa halali dhidi ya raia wa Kipalestina wasio na silaha na mali zao katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi yanayokaliwa kwa mabavu na Israel.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini New York siku ya Ijumaa, Guterres alisisitiza umuhimu wa kutekeleza sheria za kimataifa, ikiwemo kanuni za sheria za kibinadamu na haki za binadamu, katika maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, ikiwemo Mashariki mwa al-Quds.
Aidha, alieleza kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imeweka hatua za muda ambazo ni za lazima na lazima zitekelezwe.
Guterres amesema: “Maoni ya ushauri ya mahakama ya Oktoba 22, 2025 yalikuwa wazi: Israel ina wajibu wa kuruhusu na kuwezesha misaada ya kibinadamu, kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika utekelezaji wa majukumu yetu, na kuheshimu hadhi na kinga za Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wake, hata nyakati za vita.”
Katibu Mkuu huyo alithibitisha tena uungaji mkono wake kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), akisisitiza nafasi yake muhimu katika kuwasaidia Wapalestina, ndani ya Gaza na maeneo mengine ya Asia ya Magharibi.
Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wanakabiliwa na operesheni za kijeshi za Israel na ongezeko la mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni tangu kuanza kwa vita vya Israel dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 2023, ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 70,000, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.
Tangu wakati huo, zaidi ya Wapalestina 1,085 wameuawa na wengine 10,700 kujeruhiwa katika Ukingo wa Magharibi kutokana na mashambulizi ya jeshi katili la Israel na walowezi wa Kizayuni. Zaidi ya watu 20,500 pia wametekwa na majeshi vamizi ya Israel.
Kwa miezi kadhaa, mashirika ya haki za binadamu yamekuwa yakitoa tahadhari kuhusu hatari ya kuendelea kwa mpango wa maangamizi ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi katikati ya vurugu zinazoendelea.
Mnamo Julai 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ilitangaza kuwa uvamizi wa muda mrefu wa Israel katika ardhi ya kihistoria ya Palestina ni kinyume cha sheria na ikatoa wito wa kuondolewa kwa makazi yote ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi na Mashariki mwa al-Quds.