
Kundi la kwanza la mabasi ya umeme yaliyotengenezwa nchini Iran limeanza kutoa huduma katika mji mkuu, Tehran, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mfumo wa usafiri wa umma na kupunguza uchafuzi wa hewa unaosababishwa na mabasi ya dizeli ya kizamani.
Naibu Meya wa Tehran, Mohsen Hormozi, amehudhuria hafla ya kuzindua mabasi mapya matano ya umeme yaliyotengenezwa na kampuni za ndani kwa ajili ya mfumo wa usafiri wa umma wa jiji.
Hormozi amesema mabasi hayo matano yatafanya kazi katika njia yenye urefu wa kilomita 4.5 katikati ya jiji la Tehran, kama sehemu ya mpango wa majaribio uliobuniwa kupima utendaji katika mazingira halisi ya kazi.
Amesema: “Ilichukua muda mrefu kukamilisha majaribio ya kiufundi kwa mabasi haya, kwa kuwa haya ndiyo ya kwanza kutengenezwa ndani ya nchi na yalihitaji kufikia uthabiti kamili wa kiutendaji.”.
Afisa huyo ameongeza kuwa mabasi mengine 25 ya umeme ya ndani yatakabidhiwa kwa manispaa ya Tehran kufikia mwisho wa mwaka wa kalenda ya Iran mnamo Machi, na mengine 25 kufikia Mei. Amesema idadi ya mabasi ya umeme ya kutengenezwa nchini yatakayotumika Tehran inatarajiwa kufikia 100 kufikia kiangazi cha mwaka ujao.
Mabasi hayo yameundwa kwa ushirikiano wa kampuni za Iran, Oghab Afshan na MAPNA, na yanasambazwa na kampuni mpya iitwayo SHETAB na yamepewa jina la Zima. Yataungana na msafara wa mabasi 390 ya umeme yaliyoagizwa kutoka China na ambayo tayari yanahudumia abiria wa ndani ya jiji la Tehran.
Ripoti zinasema takriban mabasi mengine 110 ya umeme kutoka China yanatarajiwa kutumika Tehran mara tu baada ya kukamilisha taratibu za forodha katika bandari za kusini mwa Iran.
Uanzishaji wa mabasi ya umeme ni sehemu ya mpango mpana katika Tehran na miji mingine mikubwa ya Iran wa kuboresha mifumo ya usafiri wa umma na kupunguza uchafuzi wa hewa kutoka kwa magari ya kawaida.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kutoka Shirika la Ulinzi wa Mazingira la Iran, magari yanachangia hadi asilimia 80 ya uchafuzi wa hewa mjini Tehran, jiji linalokumbwa na viwango vya juu vya uchafuzi hasa mwanzoni na katikati ya msimu wa vuli.